Mkuu wa Bandari ya Kyela, Percival Salama
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa meli tatu za kisasa katika Ziwa Nyasa.
Kati ya meli hizo tatu, mbili zitasafirisha mizigo na moja itasafirisha mizigo na abiria. Ujenzi wa meli hizo unafanyika katika bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya, ambako meli za mizigo zinatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu na ile ya abiria na mizigo, inatarajia kukamilika Februari mwakani.

Mkuu wa Bandari ya Kyela, Percival Salama alisema kwamba miradi ya ujenzi wa meli hizo unaotekelezwa na Kampuni ya M/s Songoro Marine Transport Ltd ni wenye tija na faida kubwa kwa TPA na taifa kwa ujumla.
“Meli hii (akionesha ile ya abiria) inayojengwa katika bandari yetu ya hapa Itungi ni ya kisasa kama mnavyoiona na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na shehena ya tani 200, pamoja na magari kwa wakati mmoja,” alisema Salama kwa mujibu wa taarifa ya TPA.
Akizungumzia uundaji wa meli mbili za mizigo, Salama alisema mradi huo wa uundaji wa meli hizo mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja, unaendelea vizuri na kwa sasa umefikia asilimia 80 ya utekelezaji wake.
Kuhusu miundombinu, Salama alisema kwamba ujenzi wa gati la kuegeshea meli katika Bandari ya Kiwira na Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Bandari hiyo umekamilika.
“Gati hii la abiria na mizigo lililojengwa katika bandari yetu ya Kiwira lina uwezo wa kuegesha meli mbili kwa wakati mmoja,” alisema Salama.
Katika kuhakikisha TPA inaboresha huduma za kibandari katika Ziwa Nyasa, imekamilisha ukarabati wa pantoni tano kupitia mradi wa chelezo liliwekwa bandari ya Itungi zitakazowekwa katika bandari za Ziwa Nyasa ili zitumike kuboresha huduma kwa abiria na mizigo.
“Aidha, kwa sasa TPA ipo katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa gati katika bandari ya Ndumbi litakalotumika kuhudumia abiria na mizigo. Gati hilo linatarajia kukamilika mwezi Machi, 2017,” alisema.
Akizungumzia faida za ujenzi wa meli hizo katika Ziwa Nyasa, Salama alisema ni pamoja na kufungua fursa kubwa ya kukuza na kuboresha shughuli za kiuchumi, kibiashara na kijamii katika ukanda wa Ziwa Nyasa hasa katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Ruvuma na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia; kuongeza mapato kwa TPA na kwa nchi.
“Hii inatokana na ukweli kwamba wateja wengi wameonesha utayari mkubwa katika kutumia usafiri wa njia ya maji mara vyombo hivyo vitakapokamilika,” aliongeza.
Akizungumzia suala la kuongezeka kwa ajira, alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja; na kwamba miradi hii pia ni kichocheo kizuri cha kufunguka kwa Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara hivyo kuzifanya Bandari za Mtwara na Mbamba Bay kuhudumia soko la Malawi na hivyo kupunguza ushindani wa Bandari za Msumbiji kwa Bandari ya Dar es Salaam.
“Hii itaifanya pia Bandari ya Mtwara kuwa na kazi nyingi wakati wote wa mwaka tofauti na sasa ambapo inakuwa na kazi nyingi kipindi cha mavuno ya korosho tu,” alifafanua.
Akielezea uboreshaji wa miundombinu ya kibandari katika ziwa Nyasa, alieleza kuwa mamlaka imeingia mkataba wa miezi tisa kuanzia Juni 30, mwaka huu na Kampuni ya OCKPA ya kuweka “heavy paving” katika bandari za Itungi na Kiwira. Salama alisema katika ziwa Nyasa, TPA inasimamia, kuendesha na kuendeleza jumla ya bandari 15.
Bandari hizo ni Itungi, Kiwira na Matema zilizopo Kyela; Ndumbi, Lundu, Mkili, Njambe, Liuli na Mbamba Bay zilizopo Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde, Lupingu na Manda zilizopo Ludewa mkoani Njombe.
Aina ya mizigo inayohudumiwa katika bandari za ziwa Nyasa ni makaa ya mawe, mbolea, saruji, mbao, mihogo, mahindi, dagaa, bati na mizigo mingine mchanganyiko. Bandari hii inalenga kuwa lango la kuhudumia shehena kutoka na kwenda mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma na nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji.