SabodoMustafa Jaffer Sabodo
DAR ES SALAAM: Jumanne iliyopita ilikuwa ya gumzo kuhusu tamko la mfanyabishara  maarufu Bongo, Mustafa Jaffer Sabodo kusema atatoa kiasi cha shilingi trilioni 10 (dola za Marekani bilioni 5) kwa ajili ya uwekezaji mkoani Dodoma kwa lengo la kumuunga mkono Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ kuhamisha makao makuu ya serikali kwenda mkoani humo.
Sabodo alisema kuwa, utendaji wa JPM umemvutia kutokana na hatua yake ya kupiga vita rushwa na ufisadi na akatangaza kuwa kuanzia sasa hatatoa tena msaada kwa vyama vya upinzani kama alivyokuwa akifanya miaka ya nyuma.
LAKINI AANIKA MASHARTI
Akizungumza jijini Dar es Salaam Jumatatu iliyopita, Sabodo alisema atawekeza kiasi hicho cha fedha iwapo serikali yote itahamia Dodoma kwani itakuwa ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa, hayati  Mwalimu Julius Nyerere aliyetamani kuona mkoa huo unakuwa makao makuu ya nchi miaka 43 iliyopita.
Noti-BandiaMANENO YA SABODO
“Niliposikia anatangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba, serikali itahamia Dodoma ilikuwa mara yangu ya kwanza baada ya miaka mingi kupita. Nilitabasamu moyoni jambo ambalo lilinitokea miaka 10 ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Nyerere,” alisema Sabodo alipoongea na wanahabari.
GUMZO LENYEWE
Baada ya tamko lake, wasomaji wengi wa Magazeti Pendwa ya Global walipiga simu chumba cha habari wakitaka kujua asili ya utajiri wa Mtanzania huyo mpaka kufikia hatua ya kuwekeza kwa kiwango hicho kikubwa cha pesa.
“Jamani huyu Sabodo mbona ni tishio, uwekezaji wa trilioni moja si mchezo. Hivi mbona huyu mtu hayupo kwenye orodha ya matajiri wa Tanzania. Mimi ninavyojua hizo pesa ni za bajeti ya wizara kadhaa za Bongo,” alisema mama Mkwepu, mkazi wa Mbezi Beach, Dar.
MBONGO AZIPIGIA HESABU
Juliana Julius, mkazi wa Magomeni jijini Dar naye alisema kuwa, alishtuka kusikia mfanyabiashara huyo akitamka kuwekeza kwa pesa nyingi kiasi hicho.
“Unajua ilifika mahali mimi mwenyewe nikapiga hesabu. Watanzania tupo milioni kama hamsini, ukimgawia kila mtu katika trilioni kumi, kila mmoja atapata laki mbili mfukoni mwake. Da! Kiu yangu kubwa mimi ni kumjua huyu Sabodo ni nani hasa hapa nchini!”
Siku ya Jumanne, mapaparazi wetu walipokuwa wakipita kwenye sehemu zenye mikusanyiko ya watu, wengi walikuwa wakimzungumiza Sabodo na uwekezaji wake wa shilingi trilioni kumi. Wengine waliamini, wanahabari walikosea kuchukua maelezo yake, kwamba, alisema shilingi bilioni kumi na si trilioni.
“Mimi jamani nawaambia, mtasikia alikosea, kweli tena. Hivi mnajua trilioni kumi ni nyingi sana? Aisee huyu mtu ana pesa balaa,” alisikika akisema abiria mmoja kwenye Kituo cha Basi cha Mwendokasi, Ubungo jijini Dar.
AMANI OFISINI KWA SABODO
Ili kumjua kwa undani zaidi, juzi, mapaparazi wetu walifunga safari hadi ofisini kwa mfanyabiashara huyo Mtaa wa Uhuru na Nkrumah, Mnazi Mmoja, Dar kwa lengo la kuzungumza naye kwa kirefu asili yake na maisha yake kwa ujumla.
Hata hivyo, mtu mmoja aliyekutwa mahali hapo ambapo pana duka kubwa, alisema Sabodo hakuwepo, lakini kwa urahisi sana anapatikana Upanga mapema asubuhi. Mapaparazi wetu wanaendelea kumfuatilia.
HISTORIA KWA UFUPI
Sabodo ni mfanyabiashara Mtanzania mwenye asili ya Kihindi aliyezaliwa mkoani Lindi. Katika maisha yake amekuwa akifanya biashara kwenye nchi za Kenya, Ufaransa, India, Sudan na Zimbabwe.
Pamoja na biashara zake, Sabodo amekuwa anajihusisha kuchangia miradi ya maendeleo ya huduma za jamii, uimarishaji wa demokrasia nchini na pia alishiriki kutunisha mfuko wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha bahati nasibu ya kutolewa fedha ya kuongezeka papo kwa papo kwa ajili ya mauzo  ya shilingi milioni 100.
Katika mfuko wa Mwalimu Nyerere, Sabodo alichangia shilingi milioni 800.
Ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mfandhili mkubwa wa chama hicho.
Mwaka 2009-2010, Sabodo alikichangia Chama cha Demekrasia na Maendeleo (Chadema) zaidi ya shilingi milioni 200.
MATAJIRI WA BONGO MPAKA SASA
Kwa mujibu wa mitandao, mpaka mwaka jana, matajiri wa Tanzania ni  Saidi Bakhresa, Gulam Dewji, Rostam Aziz, Reginald Mengi, Ali Mufukuri, Abdul Aziz Abood, Yusuf Manji na wengineo. (orodha hii si katika mpangilio wa moja na kuendelea).