Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewatoa hofu wananchi kuwa hakutakuwa na uvunjifu wa amani kutokana na sintofahamu inayoendelea nchini baina ya vyama vya siasa.

Alisema suala hilo litajadiliwa kwa njia ya busara na amani kwa kufanya mazungumzo na kamwe wananchi wasiaminishwe kuwa kuna ombwe la utendaji na kwamba hakuna njia ya suluhu katika masuala ya siasa.
Jaji Mutungi ambaye ni Mlezi wa Vyama vya Siasa nchini, amevisihi vyama vyote vyenye mipango ya kufanya mikutano au maandamano wasubiri yafanyike kwanza mazungumzo mapema wiki ijayo ili upatikane ufumbuzi unaostahili.
Aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa Baraza la Vyama vya Siasa limeitisha mkutano maalumu kujadili changamoto na kuhakikisha wanamaliza sintofahamu iliyopo.
Alisema kikao hicho cha siku mbili kitatanguliwa na Kamati ya Uongozi itakayokaa na kupanga namna ya kufanya majadiliano hayo na kufikia muafaka.
Jaji Mutungi alisema kikao hicho kitafanyika Agosti 29 na 30, mwaka huu, na wamealika wageni mbalimbali kuzungumzia masuala hayo yaliyojitokeza na kuleta sintofahamu ili kuepuka nchi kuwa mfano wa kusema yalijitokeza haya kutokana na kutoelewana.
“Kwa kikao hiki cha baraza ambacho kitashirikisha wanachama wake kutoka vyama vyote vya siasa watafanyia kazi sintofahamu zilizojitokeza na kufikia muafaka hivyo wananchi hawatakiwi kuwa na hofu,” alisema Jaji Mutungi.
Hivi karibuni, kumeibuka taharuki miongoni mwa wananchi kuhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza operesheni mpya iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) ambayo itaanza kwa maandamano nchi nzima Septemba mosi, mwaka huu.
Kutokana na kutangaza operesheni hiyo itakayofanyika kwa kuandaa mikutano ya hadhara na maandamano, Rais John Magufuli aliingilia kati na kupiga marufuku kwa kuwaasa kutomjaribu kwa kufanya operesheni hiyo jambo lililoungwa mkono na Msajili huyo.
Lakini Chadema imeendelea kusisitiza kufanyika kwa maandamano na mikutano hiyo ambayo pia imepigwa marufuku na Jeshi la Polisi ambalo katika siku za karibuni limeonekana likifanya mazoezi ambayo wananchi wameyaelezea kuwa ni kupambana na watakaoshiriki katika operesheni hiyo.
Jaji Mutungi aliongeza kuwa yeye kama mshiriki atapata nafasi ya kuzungumzia mambo yaliyosababisha sintofahamu ikiwa ni pamoja kuzuiwa kwa shughuli za vyama vya siasa na nini Katiba inasema pamoja na changamoto nyingine kwa lengo la kutoa ufafanuzi.
Akizungumzia changamoto ya kutohudhuria kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, Msajili huyo alisema kwa kuwa baraza ni la vyama vyao, ana hakika vyama vyote pamoja na wadau wengine watashiriki.
Aidha, alisema kuhusu migongano iliyojitokeza katika Chama cha Wananchi (CUF) wakati wa mkutano wake maalumu, alieleza kuwa muda ukifika atalizungumzia hilo.
Alizungumzia pia azma ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kuandamana nchi nzima kwa lengo la kumpongeza Rais Magufuli kuwa hajapata taarifa rasmi kutoka UVCCM na akishapata atatolea tamko.
Wakati huo huo, Chadema imesema imeupokea mwito wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini juu ya kuwa na mazungumzo ya pamoja na kusema kuwa mjadala huo ukifanywa kwa umakini utakuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, Dar es Salaam jana, ilisema wameusikia mwito huo uliotolewa na Jaji Mutungi wa kuitisha meza ya majadiliano na mazungumzo ambayo iwapo yatatawaliwa na nia njema na dhamira safi ya kuheshimu Katiba ya Nchi.
“Tumeusikia wito wake wa kuitisha meza ya majadiliano na mazungumzo ambayo iwapo yatatawaliwa na nia njema na dhamira safi ya kuheshimu Katiba ya Nchi na utekelezaji wa sheria za nchi bila kupindisha pindisha, hususan Sheria ya Vyama vya Siasa, yanaweza kuwa na manufaa kwa Watanzania wote,” alisema Makene.
Aidha, Chadema kupitia msemaji wake huyo wamelituhumu Jeshi la Polisi kwa kile alichosema kuingilia vikao vya ndani vya chama hicho na kuzuia visiendelee na kuwa ni kinyume cha sheria na taratibu za mamlaka yao.
Alisema licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kufanya jitihada hizo, lakini Polisi linashikilia watu mbalimbali, wakiwemo wafuasi, mashabiki, wanachama, viongozi wa Chadema kwa kushiriki katika vikao hivyo wakitekeleza wajibu na haki zao za kikatiba na kisheria.
“Wakati tunasubiri meza ya mazungumzo kupitia Baraza la Vyama, tunapenda kusisitiza kuwa Chadema itasimama imara kuhakikisha misingi ya demokrasia na utawala unaozingatia katiba na sheria unafuatwa,” alisema Makene.