Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Maseru
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imepanga kuanzisha huduma za matibabu ya figo na sikio kati ya Desemba mwaka huu na Januari mwakani. Itaanzisha huduma hiyo kwa lengo la kuhakikisha inapunguza gharama na idadi kubwa ya wagonjwa wanaoenda nje ya nchi, kutafuta huduma za matibabu.

Akizungumza katika kipindi cha Funguka, kinachorushwa na televisheni ya Azam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Maseru, alisema Septemba mwaka huu, madaktari bingwa wataenda India kwa ajili ya kupatiwa mafunzo kwa ajili ya huduma hizo za matibabu.
Alisema hatua hiyo, imetokana na dhamira ambayo hospitali hiyo imejiwekea ya kuhakikisha huduma zote muhimu za matibabu, zinapatikana katika hospitali hiyo ili kuwapunguzia Watanzania gharama za matibabu kutoka hospitali za nje.
Alikiri kuwa hospitali hiyo imekuwa ikishuhudia idadi kubwa ya wagonjwa wenye matatizo ya figo na masikio, wanaoenda nje ya nchi, kufuata huduma ya matibabu, hatua inayoigharimu serikali fedha nyingi.
Akizungumzia huduma ya tiba ya masikio, alisema ni kitendo cha kuweka kifaa cha elektroniki sikioni kwa ajili ya kuwasaidia wenye matatizo ya kusikia. “Huduma hii kwa kawaida operesheni yake inagharimu takribani Sh milioni 100 kwa masikio yote mawili,” alisema.
Alisema madaktari bingwa watakaokwenda India kwa ajili ya mafunzo zaidi kuhusu huduma hizo, watapatiwa mafunzo hayo kwa miezi miwili na pindi watakaporejea ndipo huduma hizo rasmi zitaanza kutolewa katika hospitali hiyo ya MNH.
Alisema huduma ya tiba ya masikio ikianzishwa nchini itasaidia watoto na watu wazima wenye usikivu hafifu au wasiosikia kabisa kuwa na uwezo wa kusikia na hivyo kuweza kuendelea na shughuli zao za kawaida ikiwemo kuhudhuria shule za kawaida.
Kuhusu huduma ya kubadilisha figo, Profesa Maseru alisema hospitali hiyo imekuwa ikipokea pia wagonjwa wengi wenye matatizo ya figo, ambapo wapo wagonjwa takribani 100 wanapatiwa huduma ya kusafishwa figo na wengine zaidi ya asilimia 80 wanahitaji operesheni ya kuwekewa figo mpya.
Huduma ya chakula Akizungumzia suala la mfumo mpya wa kutoa chakula hospitalini na mgonjwa kuchangia gharama, uliositishwa na Serikali, Profesa Maseru, alisema huduma hiyo itaanza tena upya hivi karibuni baada ya serikali kuitaka hospitali kujipanga upya.
“Si kuwa utaratibu huu umesitishwa ila tumeambiwa tujipange upya na hivi karibuni tutaanza kutoa hicho chakula kupitia kwa mzabuni kwa awamu. Tutaanza na kutoa chakula kwa wagonjwa ambao hospitali ndio inawagharamia chakula tuone changamoto zitakazokuwepo,” alisisitiza.
Alisema endapo utaratibu huo, utaenda vizuri, hospitali itaandaa ripoti na baada ya miezi sita itajadiliana na wizara kuona namna ya kutekeleza vyema mfumo huo mpya.
Alisema kwa kawaida hospitali nyingi duniani hutoa chakula kwa wagonjwa wanaolazwa, ila kwa hapa nchini utaratibu huo ulibadilika katika miaka ya 1990 kutokana na hali ya uchumi na ndugu ndio walioachiwa wajibu huo.
Alisema MNH kwa sasa ina takribani wagonjwa 13,000 wanaolazwa kwa siku kati ya hao, hospitali hiyo huwapatia chakula wagonjwa 600 hadi 700 wanaotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumzia uhaba wa madaktari, alisema pamoja na kwamba kuna takribani vyuo saba vinavyozalisha madaktari nchini, bado idadi ya madaktari wanaohitimu kwa mwaka ambao ni 1,500 haitoshelezi mahitaji.
Alisema kwa sasa Tanzania ina wastani wa madaktari mmoja kwa wagonjwa 18,000 wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) viwango vyake vinataka angalau daktari mmoja kwa wagonjwa 10,000.