Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametoa siku saba kuanzia jana kwa vyuo vikuu nchini, ambavyo vimepokea fedha za mikopo za wanafunzi ambao hawapo chuoni, kurejesha fedha hizo.
Aidha, amesitisha mikopo kwa wanafunzi wote 2,192 ambao walipuuzia kuhakikiwa hata kama wapo wenye sifa hadi pale watakapojaza upya fomu za kuomba mikopo, kwa kuwa wamekaidi agizo la serikali.

Profesa Ndalichako alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, akitoa taarifa ya kazi ya uhakiki wa wanafunzi wanufaika wa mikopo kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini.
Alisema katika uhakiki huo kwa mara ya kwanza wanafunzi 2,763 hawakujitokeza, baada ya taarifa hiyo kutolewa kwenye vyombo vya habari na majina yao kuwekwa hadharani, awamu ya pili na ya tatu walijitokeza wanafunzi 571 na kuhakikiwa.
“Uhakiki wa malipo yaliyofanyika unaonesha kuwa wanafunzi hao 2,192 ambao hawakujitokeza kuhakikiwa wameigharimu serikali kiasi cha Sh 3,857,754,460 kwa mwaka wa fedha 2015/2016,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema uhakiki huo ulifanywa kwa vyuo vya elimu ya juu 31 kati ya 81 vilivyopo nchini na kwamba kazi hiyo ilifanywa kwa awamu tatu mfululizo, baada ya wizara kuunda timu ya kuhakiki wanafunzi kwenye taasisi za elimu ya juu nchini ili kuiridhisha na uhalali wa wanafunzi wanaopata mikopo kwa ajili ya elimu ya juu.
“Uhakiki ulifanywa na watumishi wa Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kati ya mwezi Mei hadi Julai mwaka huu. Wanafunzi wanufaika wa mikopo walitakiwa kujitokeza na kuonana na timu ya uhakiki ana kwa ana ili kutambuliwa na kuhakikiwa,” alieleza.
Baadhi ya idadi ya wanafunzi wa chuo ambao hawakuhakikiwa na kiasi cha fedha walicholipwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) idadi ya wanafunzi wasiohakikiwa 350, fedha zilizolipwa kwa wasiohakikiwa Sh 703,438,635, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wanafunzi 364, Sh 460,963,550, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Dar es Salaam wanafunzi 200, Sh 408,854,325, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), wanafunzi 235, Sh 387,625,650, Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), wanafunzi 84 Sh 146,190, 775, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IMF), wanafunzi 85, Sh 147,314,075 na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU), wanafunzi sita, Sh 14,160,000.
Profesa Ndalichako alisema kutokana na mambo hayo yaliyobainika, pia serikali imeviagiza vyuo vikuu kuwasilisha Bodi ya Mikopo kwa wakati taarifa zote za kitaaluma na za kibenki za wanafunzi ili kuiwezesha Bodi ya Mikopo, kufanya marekebisho stahiki katika kumbukumbu zao na kuepusha ulipaji wa fedha kwa wanafunzi wasiostahili.
Aidha, Bodi ya Mikopo imetakiwa kuchambua na kuingiza mara moja mabadiliko ya taarifa za wanafunzi kama zilivyopokelewa kutoka vyuoni ili kuepusha ulipaji wa fedha kwa wanafunzi wasiostahili. Alitaka kuchukuliwa kwa hatua kali za kinidhamu kwa wote waliohusika kufanikisha malipo kwa wanafunzi ambao hawapo vyuoni.
“Hii inahusisha wafanyakazi wa bodi ya mikopo na vyuo husika,” alifafanua huku akivitaka vyuo kuweka utaratibu mzuri wa kudhibiti malipo kwa wanufaika wa mikopo ili kuepuka kufanya malipo kwa wanafunzi hewa. Mbali na hilo, aliwataka wakuu wa vyuo kuweka mfumo wa kuhakiki usahihi na matokeo ya wanafunzi yanayotumwa na Bodi ya Mikopo na watawajibika kwa usahihi wa taarifa zinazowasilishwa. “Kwani zoezi la uhakiki limebaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye matokeo ya wanafunzi, wapo ambao hawakufanya mtihani au waliofeli lakini wameandikiwa ‘pass’ ili waendelee kupata mikopo,” alisema.
Alisisitiza uchunguzi zaidi kufanyika kwa miaka iliyopita ili kubaini fedha za mikopo zilizolipwa kwa watu wasiostahili, akisema hatua hiyo inatokana na matokeo ya uchunguzi kubaini kuwa wapo baadhi ya wanafunzi waliohitimu tangu mwaka 2013, lakini wameendelea kupokea fedha na wengine waliofukuzwa kwa kushindwa masomo tangu mwaka 2013/2014 lakini bado wamelipwa hadi mwaka 2015/2016.