SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ametangaza rasmi kuwa watumishi karibu wote wa Bunge, watahamia Dodoma na kubainisha kuwa kutokana na serikali kuhamia mkoani humo, utaratibu wa kuendesha Bunge utabadilika siku za usoni.
Alisema hayo jana mjini hapa baada ya kuwasili kutoka jijini Dar es Salaam, ambako awali alikuwa nchini India kwa matibabu ya maradhi yanayomsumbua. Ndugai alisema baada ya serikali yote kuhamia Dodoma, taratibu za uendeshaji wa Bunge zitabadilika kwa siku za usoni.

Alisema watajadiliana na wabunge ili Bunge la Tanzania liwe kama mabunge mengine, ambayo Kamati na Bunge linaendeshwa kwa pamoja.
Alisema uamuzi wa serikali kuhamia makao makuu Dodoma, ambao ulitamkwa na Rais John Magufuli kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wao kama Bunge kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi Dodoma na makao makuu ya taasisi ya Bunge yako Dodoma.
Alisema kwa kuwa uamuzi huo umefanyika, watumishi karibu wote wa Bunge watahamia Dodoma na Dar es Salaam watabaki watumishi wachache kwa ajili ya huduma maalumu. “Bunge litaanza kufanya shughuli Dodoma kwa asilimia zote mia kwa shughuli za Kamati na vikao vya Bunge zima,” alieleza.
Alipohojiwa suala la Ukawa katika vikao vya Bunge na kutokuwa na imani na Naibu Spika na maspika wastaafu kufanya usuluhishi ili kupata muafaka, Ndugai alisema, “Ndio nawasili, wabunge wenzangu wanaanza kuwasili, nina hakika timu itakapokamilika wabunge wote wakiwa wamekamilika wa CCM na upinzani, nina hakika tutatafuta njia ya kufanya kazi kwa pamoja.”
Alisema kinachomgusa, si suala la wabunge wa upinzani kutoka nje, kwani hilo ni jambo la kawaida, au la mbunge mmoja mmoja anasaini anatoka, kwani kuna wabunge hata wa CCM waliokuwa wakitoka nje kivyao. Lakini, alisema shida kubwa anayoiona ni wabunge kutokuwa na mahusiano mazuri, kazi ya yale wa CCM na wa Upinzani.
“Tatizo langu mimi ningependa tuelewane na wabunge, ilifikia mahali mahusiano ya wabunge wa pande hizi mbili yalikuwa mabaya mno, kama mnakumbuka sehemu kubwa ya kipindi kile kilikuwa ni mwezi wa Ramadhani, ilifika mahali hata mtu fulani akitengeneza futari watu wa upande fulani hawawezi kwenda kula futari ile,” alisema Ndugai ambaye kwa muda mrefu hakuwapo katika uongozi wa mhimili huo wa Dola, akiwa India kwa matibabu.
Pia alisema wengine hawasalimiani, wakawa na uadui, wengine wanaenda kanisa moja au msikiti moja, wakitoka pale hawasalimiani. Mbunge anasalimia watu wengine na hamsalimii mbunge mwenzake, anamuacha katika mazingira hayo ya chuki kubwa kiasi hicho.
Alisema hayo mazingira hayapendezi, wabunge ni timu moja na ushirikiano katika kazi ni lazima ujengwe na udumishwe.
Alisema serikali imesema mawaziri na makatibu wakuu wanahamia Dodoma hivi karibuni, hao ndio wanaowahitaji mno kwenye vikao vya Kamati za Bunge, suala la gharama litapungua zaidi sasa kuliko ilivyokuwa nyuma, kwa vile watumishi wote walikuwa Dar es Salaam.
Aidha, alisema Kanuni za Bunge zinapaswa kutazamwa upya katika baadhi ya maeneo kwa sababu zimetungwa mwaka 2007.
Alisema hilo linawezekana kwa sababu zimetungwa na wabunge wenyewe. Alisema katika mabunge mengine, kila Bunge la zamani linapomalizia muda linapitia kanuni mpya, Bunge linalokuja watu wapya linakuta kanuni zilizorekebishwa na waliooondoka.