WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amevitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinaandika habari za kina za kilimo, ufugaji na uvuvi ambazo zitawasaidia wakulima kufanya shughuli zenye tija.
Nape aliyasema hayo baada ya kukagua mabanda kadhaa, likiwemo la Kampuni ya magazeti ya Serikali ya Tanzania Standard Newspapers Limited (TSN) kwenye Viwanja vya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, Ngongo Lindi.

Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kuelimisha wakulima, wafugaji na wavuvi, elimu itakayowasaidia kuzalisha mazao yaliyo bora na upatikanaji wa masoko.
“Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli imekuwa na msisitizo wa kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na malighafi za viwanda hivyo ni mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, hivyo ni lazima watu hawa wapate taarifa sahihi,” alisema.
Aidha, alisema Maonesho ya Nanenane ya Ngongo, yamekuwa yakiimarika siku hadi siku na kuwataka wakulima kutumia fursa hiyo, kupata taarifa sahihi za sekta zao ili kuimarisha mazao yao.
Nape alitumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi za umma, kuhakikisha zinajenga majengo imara na kuachana na majengo ya muda ili yatumike wakati wa maonesho mengine.
Pamoja na kuipongeza TSN kwa kuwa na banda katika maonesho hayo, aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inatangaza gazeti mtandao lake (online publication), lifahamike kwa jamii ili walitumie kupata taarifa mbalimbali.
Akitoa maelezo ya suala hilo, mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa TSN, Prosper Mallya alisema kwa sasa gazeti mtandao linapatikana na kwamba kwa sasa kazi ya kulitangaza inafanywa na Kampuni ya Vodacom.
Alisema kupitia gazeti mtandao, TSN inaweza kuwafikia watu wengi ndani na nje ya nchi, ambao hawawezi kupata nakala halisi ya gazeti, lakini wanaweza kusoma na kupata habari sahihi zilizoandikwa kwa weledi.