Mkurugenzi wa Mahusiano wa SBL John Wanyancha ( kulia)   akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) Wakati wa kutangaza mpango kampuni hiyo wa kugharamia elimu ya vyuo vikuu kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zisizo na uwezo ili kuwapa walengwa fursa ya kutimiza malengo na ndoto zao za kimaisha.Pembeni yake ni Meneja wa Miradi ya Jamii wa SBL Hawa Ladha katika mkutano uliofanyika mapema leo katika ofisi za SBL,Temeke  jijini Dar es salaam.

Meneja wa Miradi ya Jamii Hawa Ladha akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati wa kutangaza mpango wa kampuni hiyo kugharamia elimu ya vyuo vikuu kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zisizo na uwezo ili kuwapa walengwa fursa ya kutimiza malengo na ndoto zao za kimaisha,kulia kwake ni Mkurungezi wa Mahusiano wa SBL John Wanyancha katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mapema leo katika ofisi za SBL zilizopo Temeke Jijini Dar es salaam.

Waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini mkutano huo mapema leo asubuhi katika ofisi za SBL zilizopo Temeke jijini Dar es salaam.


Dar es Salaam, Agosti
18, 2016 - 
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa mara nyingine
imetangaza mpango wa kugharamia elimu ya vyuo vikuu kwa wanafunzi wanaotoka katika
familia zisizo na uwezo ili kuwapa walengwa fursa ya kutimiza malengo na ndoto
zao za kimaisha.

Huu ni mwaka wa sita
mfululizo ambapo SBL  inatoa msaada kwa wanafunzi wa
ndani  wanaochukua  kozi za shahada katika vyuo vikuu
vya Tanzania  chini ya programu ya kampuni ijulikanayo kama “Skills
for Life”. Jumla ya wanafunzi 31wa Tanzania tayari wameshanufaika
na  mpango huu ambao ni sehemu ya Mfuko wa Kampuni ya Bia ya Afrika
Mashariki (EABL Foundation).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi
wa Mahusiano wa SBL John Wanyancha fomu za maombi kwa ajili ya udhamini
zinapatikana katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Dar es Salaam, Moshi na
Mwanza au kupitia tovuti ya www.eablfoundation.com.

Wanyancha amesema mpango
huo uko wazi kwa wanafunzi kutoka nchi nzima ya Tanzania ambao ambao tayari
wamepata usajili wa kujiunga na vyuo vikuu nchini katika fani za Biashara,
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Uhandisi  na Sayansi ya Chakula
katika ngazi ya shahada kutoka vyuo vikuu hapa nchini.

Mfuko wa EABL
ulianza  kutoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi kuanzia wanaojiunga
na vyuo vikuu mwaka 2005 ambapo hadi sasa zaidi ya wanafunzi 238 wamenufaika
kwa mpango huo wakiwemo 31 kutoka Tanzania. Wengi walionufaika tayari
walishamaliza masomo yao  na wanafanyakazi katika makampuni
mbalimbali  katika ukanda huo. Mpango huu upo katika nchi za Kenya,
Tanzania na Uganda ambapo mfuko wa EABL umetumia jumla ya zaidi ya Tshs billion
5 kuugharamia tangu mwaka wa 2005.  

Udhamini huu hugharamia
ada ya masomo, vitabu, malazi, fedha za kujikimu na programu za ushauri kwa
waombaji watakaofanikiwa.
“Lengo letu kuu kupitia
mpango huu ni kuwawezesha waombaji  kutimiza ndoto zao maisha,”
alisema Wanyancha na kuongeza kuwa tarehe ya mwisho ya kupokea maombi  ni
Septemba 20, 2016.

Mkurugenzi huyo ametoa
wito kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini kuchangamkia fursa hiyo ili
kwa kutuma maombi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ujao.

MAHITAJI MUHIMU:  Fomu za maombi
zilizojazwa vizuri  zikiwa zimeambatanishwa na  barua ya
usajili kutoka kwa taasisi ya  elimu ya juu, udhibitisho wa hitaji la
kifedha na nakala za vyeti vya elimu ya sekondari kidato cha nne na cha sita.

































Wanafunzi ambao bado
hawajapokea barua za kusajiliwa kujiunga na vyuo vikuu na ambao wanakidhi
masharti pia wanaweza kutuma maombi.