Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.
SERIKALI imesema kwamba itahamia Dodoma katika makao makuu ya nchi kwa awamu, lakini hadi sasa asilimia 75 ya watumishi wa serikali wanaweza kuhamia baada ya tathmini kubainisha kuwa idadi hiyo ya watumishi, inaweza kupata makazi katika mji huo.
Pamoja na hayo, pia imesema kwa mujibu wa tathmini hiyo takribani asilimia 70 ya ofisi za serikali nazo zinaweza kuhamia katika mji huo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati akizungumza kwenye kipindi cha Safari ya Dodoma, kilichorushwa na Kituo cha Televisheni ya TBC1 juzi.
“Hii ni kwa mujibu wa matokeo ya tathmini iliyofanywa na Kamati Maalumu ya Mkoa iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kufanyia tathmini mpango wa serikali wa kuhamia Dodoma,” alisema Waziri Jenista.
Alisema tathmini hiyo ilifanyika kwa ajili ya serikali kujiridhisha na kutambua uwezo wa mji huo, kupokea watumishi hao na ofisi za serikali ukoje huku akisisitiza kuwa pamoja na matokeo hayo, serikali itaendelea kuhamia katika mji huo ambao ndio makao makuu ya Tanzania kwa awamu.
“Lakini si kwamba serikali yote itahama kwa mara moja, hivyo muda upo wa kujipanga. Tuna majengo mengi ya serikali wala hatuendi kupanga. Hiyo asilimia 70 ni pamoja na majengo ya serikali yaliyopo katika mji huo. Lipo jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bodi ya Mfuko wa Barabara, Jengo la Mkuu wa Mkoa,” alisema.
Alisema serikali inayo uwezo wa kujipanga kwa awamu itakazojiwekea, lakini majengo ya kuanza kuipokea sehemu ya serikali hiyo, kwa sasa yameshabainika na kuthibitishwa kuwa yapo.“Hii ni wazi sasa kuwa safari ya Dodoma imeanza,” alisema.
Hata hivyo, Waziri huyo alisisitiza kuwa serikali hiyo haiwezi kuhamia katika mji huo kwa mara moja na kwamba itahamia kwa awamu ndani ya miaka minne ijayo.
Alisema kamwe Serikali ya Awamu ya Tano haijakurupuka kuanza kuihamisha serikali Dodoma kwa kuwa, suala hilo, lilikuwa kwenye mipango ya serikali zote zilizopita ikiwemo Ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka jana.
“Huu sio uamuzi wa kukurupuka, wakati wa kampeni tulinadi Ilani ya Uchaguzi, Ibara ya 151 imeandikwa kabisa kuhamishia makao makuu ya serikali Dodoma. Naamini hata Watanzania wengine walitupigia kura kwa sababu waligundua kuna kipengele cha kuhamishia serikali katika mji huu,” alisema. Alisema Rais John Magufuli alisema wazi kuwa akichaguliwa kushika madaraka atatekeleza ilani ya uchaguzi.
“Sasa tunaona kabisa kwa vitendo Rais akifanya hilo, kwa mfano kutoa elimu bure. Mbona watu hawahoji kuwa tumekurupuka katika kutoa elimu bure. Ipo ndani ya ilani. Yale yote yanayotekelezwa na serikali yamo kwenye Ilani ya CCM sio kuwa tunakurupuka,” alifafanua. Alisema mpango huo hautoathiri taratibu zozote na mipango ya maendeleo ikiwemo bajeti.
“Jambo hili halina mkono kwenye bajeti iliyokwisha kupangwa ya mwaka wa fedha 2016/17. Watu wamedai kuwa uamuzi huu utakwenda kusimamisha mipango ya maendeleo, utasimamisha bajeti isitekelezwe inavyotakiwa. Hapana si kweli,” alisema.
Aliwahakikishia Watanzania mipango yote ya bajeti itatekelezwa, kama ilivyopangwa kwa maana ya fedha za barabara, maji, dawa, elimu, afya, kilimo na maeneo mengine muhimu zitaenda kutumika kama zilivyopangwa.
“Kama tulijipanga kujenga barabara, niwaambie Watanzania barabara zile tulizojipanga kuzijenga kwa mwaka huu wa fedha tutakwenda kuzijenga, kama tulipanga kupeleka dawa tutakwenda kuzipeleka kama tulivyopanga kwenye bajeti,” alieleza.
Alisema tayari serikali imeanza kuweka mipango ya kutekeleza vyema mpango huo wa kuhamia Dodoma, kupitia kikao cha Tume ya Rais ya kuendeleza makao makuu ya nchi Dodoma kilichoundwa tangu mwaka 1984 ambacho Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu.
Alisema kupitia kikao hicho mpango kabambe wa kuhamia Dodoma uliundwa, ikiwemo kuundwa pia kwa kamati maalum ya mkoa kwa ajili ya kufanyia tathmini mpango mzima wa kuhamia Dodoma.
“Pia tumefanya kikao cha Baraza la Kazi la Mawaziri ili kuona utekelezaji wa jambo hili bila kuharibu jambo lingine lolote na sisi ndani ya Baraza tumekubaliana tunakwendaje,” alisema.
Alieleza faida za serikali kuhamia Dodoma kuwa ni pamoja na kuongeza mapato kwa serikali, kwani kwa sasa asilimia 70 ya mapato ya serikali inapatikana katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee, hivyo endapo mji wa Dodoma utapanuka zaidi, utakuwa na fursa na wenyewe kuongeza mapato zaidi kwa serikali.
Alisema serikali ikihamia Dodoma, mzunguko wa fedha katika mji huo utaongezeka, kutakuwa na fursa nyingi za ajira na uwekezaji ukiwemo kuiimarisha kiuchumi miji yote ya jirani na mji huo kama vile Iringa, Morogoro, Singida na Babati.
Waziri huyo, alibainisha mikakati ya kukuza mji wa Dodoma ikiwemo huduma za kijamii ambayo ni pamoja na maji, miundombinu na umeme na kubainisha kuwa kwa hali ilivyo, mahitaji muhimu yanatosheleza.
Alisema kwa upande wa huduma za maji, kiwango cha maji kilichohakikishwa kuzalishwa katika mji wa Dodoma kwa sasa ni mita za ujazo milioni 61 na kwa mujibu wa idadi ya wakazi wa mji huo ambao ni 410,956 maji yanayotumika ni mita za ujazo milioni 48.
“Kwa hiyo tuna ziada ya maji ya mita za ujazo zisizopungua milioni 15 hadi 16. Shida inayotakiwa kufanyiwa kazi ni kuchukua hatua za haraka kuhakikisha tunaunganisha maji kutoka katika maeneo ambayo maji yapo na kuyasambaza kwenye maeneo ya mitaa na ambayo watu watajenga,” alisema.
Kuhusu umeme, alisema kwa sasa mji huo, unazalisha megawati za umeme 48, lakini zinazotumika ni 25 tu, hivyo kuna akiba ya megawati za umeme takribani 23.
Aidha, kuhusu miundombinu, alifafanua kuwa serikali tayari imetenga fedha katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa yenye kiwango cha kimataifa, itakayotumika kutoa huduma ya usafiri wa mwendo kasi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa muda wa saa mbili hadi tatu.
Pamoja na ujenzi wa kiwanja cha ndege kuanza kutekelezwa kwa ajili ya upanuzi, pia Jenista alisema serikali imeanza kuchukua hatua kwa kuanza kuimarisha barabara zilizofunguliwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), kuziboresha kwenye kiwango cha lami.
“Kwa sasa tayari tumeshafungua takribani barabara mpya nne zinazounganisha mji wa Dodoma na mikoa mingine ambazo ni Dodoma-Iringa, Dodoma-Babati, Dodoma-Singida na Dar es Salaam-Dodoma,” alieleza na kuongeza kuwa hatua hiyo ya kuhamia Dodoma, pia imeungwa mkono na wanadiplomasia zikiwemo baadhi ya balozi kama vile China na Kuwait zilizoahidi nazo kuhamishia ofisi zake katika mkoa huo. “Tunachoamini ni kwamba kadri serikali inavyojipanga kupitia awamu zake na serikali inavyozidi kuhamia Dodoma, ninaamini balozi nyingine na zenyewe zitaendelea kutuunga mkono. Wengi wametuunga mkono kutufuata Dodoma tukaishi nao kule tutekeleze kwa pamoja shughuli za kidiplomasia,” alisema.
Akizungumzia historia ya serikali kuhamishiwa Dodoma, alisema safari hiyo, itamuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye kupitia Mkutano wa Chama cha Tanganyika African Union (TANU) Oktoba Mosi, mwaka 1973 ndio ulioweka azimio la kuhakikisha kwamba makao makuu ya serikali yanahamia katika mji huo.
Alisema baada ya azimio hilo, serikali zote nchini ziliweka mikakati ya kuhakikisha azimio hilo linatekelezwa kwa vitendo. “Nafikiri tumpongeze Rais Dk Magufuli kwa kufanikisha ndoto hii ya muda mrefu,” alieleza.