Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itahakikisha inalinda amani ya nchi kwa gharama zozote na kamwe haitoruhusu mwanasiasa yeyote kusababisha vurugu zitakazochochea uvunjifu wa amani.
“Hatuzuii kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wazee wa Mkoa wa Rukwa baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Alisema serikali inataka Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija, hivyo suala la kudumisha amani ni muhimu kwani vurugu zikitokea hawatakuwa na mahali pa kukimbilia na hakuna shughuli ya maendeleo itakayofanyika.
“Suala la uhamasishaji wananchi juu ya utunzaji wa amani ni la lazima hivyo viongozi wa dini na wazee kwa pamoja tushirikiane katika kukemea vitendo vya uchochezi kwa sababu vurugu zikitokea Watanzania hatuna mahali pa kukimbilia,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake kwa sababu kazi ya uongozi ni ngumu na ina changamoto nyingi. Pia aliwaagiza viongozi wa dini wa mkoa wa Rukwa kuharakisha uundwaji wa Kamati ya Amani ya mkoa huo.
Awali, Shehe wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali alisema madhehebu ya dini hayawezi kuvuruga amani ya nchi ila ana hofu na viongozi wa vyama vya siasa kutokana na vitendo vyao vya kuhamasisha vurugu.
Aliwaomba wanasiasa nchini kutovuruga amani kwani machafuko yakitokea watashindwa kufanya ibada mbalimbali ikiwemo kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitangaza kuzindua operesheni iliyoipachikwa jina la Ukuta yenye lengo la kufanya maandamano nchi nzima Septemba mosi, mwaka huu, kwa lengo la kutaka kuwasilisha malalamiko yao ikiwemo kupinga kuzuiwa kufanya mikutano ya siasa kwa sasa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilimekwishakutangaza rasmi kuzuia operesheni hiyo kwa kuinyima kibali Chadema baada ya kubaini kuwepo kwa dalili za uvunjifu wa amani katika maandamano hayo.
Katika hatua nyingine, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amewataka viongozi wote wastaafu nchini wakiwemo marais, makamu wa rais na mawaziri wakuu kuingilia kati mvutano unaoendelea sasa kuhusu operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) na kutafuta muafaka.
Kingunge aliwataka wazee hao wastaafu kwa pamoja kuungana na kuandaa mazungumzo na Rais John Magufuli ndani ya kipindi cha siku saba ili kutengeneza fursa ya kukutanisha pande mbili zinazosigana kuhusu suala zima la demokrasia na siasa nchini na hivyo kupata maridhiano.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, Dar es Salaam jana mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mwanachama mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kutokana na mvutano huo hali ya siasa nchini ni ngumu, tete na yenye utata.
“Ninawaomba wazee wenzangu, wapo marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu na hata mawaziri wastaafu tuungane twendeni kwa Rais Magufuli tuzungumze naye kuhusu hali hii na mustakabali wa nchi yetu, lakini kubwa zaidi tumshauri aitishe kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na Chadema ili kuepusha shari,” alisisitiza.
“Tuna hazina kubwa ya viongozi wastaafu wapo akina Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, John Malecela, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Frederick Sumaye na Edward Lowassa. Mbona wazee wenzangu mko kimya katika hili? Hatuwezi kuachia hali hii, nawaombeni chukueni hatua mzungumze na Rais tupate muafaka,” alisisitiza.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk Barnabas Mtokambali amewataka wachungaji wake kulinda amani ya nchi pasipo kuihusisha katika vurugu za aina yoyote ili kuwa mfano wa kuigwa na wengine.
Dk Mtokambali alisema hayo alipokuwa akitoa shukrani kwa Mungu baada ya kuchaguliwa kwa awamu nyingine kuliongoza kanisa hilo katika ofisi za Makao Makuu ya TAG, zilizopo Ubungo jijini Dar es Salaam. Aliwataka wachungaji hao watangulize kuhubiri neno la Mungu badala ya kujihusisha na siasa kwa sababu wao wanaonya serikali.
“Kinachonishangaza ni kwenye nchi za Ulaya, viongozi wa dini wameruhusu wanasiasa kufanya makanisa kama jukwaa la kufanyia kampeni,” alisema Askofu huyo.
Pia alisema wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana aliwaonya wachungaji wa kanisa lake kutojihusisha kwenye siasa kwa kuwa atakayekwenda kinyume angenyang’anywa cheti, nao walikuwa watiifu, badala yake aliwataka wamwombe Mungu awapatie viongozi bora.
Imeandikwa na Lucy Ngowi, Halima Mlacha, Dar na Mwandishi Maalumu, Sumbawanga.