Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz Mlima akiongea na wadau wa takwimu wakati wa uzinduzi wa warsha ya kitaifa kuhusu mpango wa Takwimu za Malengo ya Milenia kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi leo jijini Dar es salaam. Warsha hiyo inashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa akitoa taarifa ya ofisi yake ilivyojipanga katika kusimamia takwimu za taifa wakati wa uzinduzi wa warsha ya kitaifa kuhusu mpango wa Takwimu za Malengo ya Milenia kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi leo jijini Dar es salaam.  Warsha hiyo inashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu Afrika Kusini, Bw. Pali Lehohla akitoa maelezo kuhusu ofisi yake inavyoshirikiana na wadau mbalimbali katika kausimamia takwimu za taifa hilo wakati wa uzinduzi wa warsha ya kitaifa kuhusu mpango wa Takwimu za Malengo ya Milenia kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi leo jijini Dar es salaam. 
 Washiriki wa warsha wakifuatilia hotuba ya uzinduzi wa warsha ya kitaifa kuhusu mpango wa Takwimu za Malengo ya Milenia kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi leo jijini Dar es salaam.
Washiriki wa warsha wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa alipokuwa akitoa taarifa ya ofisi yake wakati wa uzinduzi wa warsha ya kitaifa kuhusu mpango wa Takwimu za Malengo ya Milenia leo jijini Dar es salaam.
(picha na Eleuteri Mangi, MAELEZO)

Na May Simba na Eleuteri Mangi, MAELEZO
SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imezindua mpango wa kuboresha matumizi ya takwimu sahihi katika kutekeleza malengo 17 ya dunia kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza na wadau wa takwimu jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa warsha ya kitaifa kuhusu mpango wa Takwimu za Malengo ya Milenia kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz Mlima amesema kuwa matumizi ya takwimu sahihi yataisaidia Serikali kutekeleza sera na mingo ya ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Malengo hayo ni pamoja na kutokomeza umasikini, njaa, kuimarisha afya na ustawi, Elimu bora, usawa wa jinsia, maji safi na salama, nishati mbadala kwa gharama nafuu, kazi zenye staha na ukuzaji uchumi, viwanda, ubunifu na miundombinu, na jamii endelevu.

Malengo mengine ni matumizi na uzalishajinwenye uwajibikaji, kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, kuendeleza uhai katika maji, kulinda uhai katika ardhi, amani, haki na taasisi madhubuti pamoja na ushirikiano ili kufanikisha malengo.

Dkt. Mlima amesema kuwa mpango huo uliozinduliwa utaisaidia Tanzania kufikia malengo ya maendeleo endelevu kulingana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025.

Aidha, Serikali inaendelea kusimamia kuwekeza zaidi katika ukusanyaji wa takwimu sahihi kwa lengo la kuweka, kufuatilia na kutekeleza mipango yake kwa kulingana na malengo iliyojiwekea. 

“Hatua hii itasaidia kuendeleza malengo ya SDG kupitia upatikanaji wa takwimu kwa njia ya uwazi ambayo itakuwa ya haraka kutuonyesha mapungufu na hivyo kutatua changamoto zinazoikabili jamii” Dkt. Mlima
Dkt. Mlima amezitaka Wizara, Taasisi na Mashirika mbalimbali kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha uwepo wa usimamizi thabiti katika kupima matarajio ya maendeleo yanayokusudiwa. 

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa lengo la warsha hiyo ni kuja na mipango ambayo itahusisha matumizi sahihi ya takwimu zitakazoisaida Serikali kutatua changamoto zilizopo na kutoa mwelekeo katika kutekeleza sera za nchi.

Vilevile, Dkt. Albina amesema kuwa, mpango huo utahusisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ambapo wamependekeza kuwepo kwa kamati itakayohusisha viongozi wa juu wa Serikali na kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu au Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi kwa kuwa wapo kwenye ngazi ya maamuzi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu Afrika Kusini, Bw. Pali Lehohla amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika suala la takwimu na kushauri mataifa mengine ya Afrika kujifunza namna  Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyopaswa kuongozwa na uongozi bora na imara.