RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj
Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa taarifa rasmi ya Serikali kuhusu kifo cha Rais
Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi.
 


Katika taarifa hiyo aliyoitoa
kupitia vyombo vya habari, Alhaj Dk. Shein kwa masikitiko makubwa aliwaarifu
wananchi kuwa leo tarehe 14 Agosti 2016, Mzee Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi
amefariki dunia, msiba ambao umetokea nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni, Dar es Salaam.


Alhaj Dk. Shei alieleza
kuwa Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili,
ambaye vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ambapo Marehemu Mzee Aboud Jumbe amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu
kutokana na umri wake. 


Kwa taarifa ya Alhaj
Dk. Shein, maziko ya marehemu yatafanyika kesho tarehe 15 Agosti 2016 saa 7.00
mchana ambapo maiti yake itasaliwa katika Masjid Mshawar, Mwembeshauri na
kuzikwa nyumbani kwake Migombani. 


Aidha, Alhaj Dk. Shein
alieleza kuwa kufuatia mchango na juhudi kubwa ambazo Marehemu Mheshimiwa Aboud
Jumbe Mwinyi alizichukua katika uhai wake kwa kuitumikia, kuiongoza na kuijenga
Zanzibar pamoja na nafasi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nchi yetu imekabiliwa
na msiba mkubwa kwa kigfo cha kiongozi huyu mahiri”alieleza Alhaj Dk. Shein
katika taarifa hiyo. 


Kutokana na msiba huo
mkubwa Alhaj Dk. Shein alitangaza rasmi siku saba za maombolezo, kuanzia kesho
tarehe 15 Agosti 2016 ambapo katika kipindi hicho chote bendera zote  zitapepea nusu mlingoti. 


Pamoja na hayo, Alhaj
Dk. Shein alieleza kuwa utaratibu wa maziko utafuata wasia ambao mwenyewe
marehemu aliutoa wakati wa uhai wake. 

“Tunaungana na
Wanafamilia wote katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Naomba kutumia nafasi
hii kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie
kauli thabit marehemu mzee wetu na amlaze pahala pema peponi, Amin. Inalillahi
wainnailaihi rajiun” Alieleza Alhaj Dk. Shein katika Taarifa hiyo.