Katibu wa TUCTA, Nicholas Mgaya
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limesema linaunga mkono suala la serikali kuhamia Dodoma na kutaka wafanyakazi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha azma hiyo ya serikali, inafanikiwa bila vikwazo.

Katibu wa TUCTA, Nicholas Mgaya alisema hayo jana mjini hapa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), ambao utaambatana na uchaguzi wa viongozi wake.
Alisema azma ya serikali kuhamia Dodoma, ilikuwepo tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza.
“Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitamka tuhamie Dodoma na wazo hilo likapitishwa kwa kura nyingi. Nchi ya Nigeria walikuja kujifunza kwetu na tayari wamehamia Abuja,” alisema.
Alisema wale ambao sasa wanasema serikali imechelewa kuhamia Dodoma wana sababu zao.
“Wakati Mwalimu Nyerere akitamka kwa mara ya kwanza serikali kuhamia Dodoma hakukuwa na wasomi wengi kama ilivyo sasa, kama shirikisho tunaunga mkono suala la serikali kuhamia Dodoma na wafanyakazi wote wanatakiwa kuunga mkono juhudi hizo,” alisema.
Alisema serikali yote itakapokuwa imehamia Dodoma na TUCTA, itahamia rasmi mkoani humo kwa vile wana jengo la ofisi na wamejenga nyumba 22 ambazo wamepangisha.
“Kwenye ofisi yetu pale Makole tuna eneo kubwa linaloweza kujenga ofisi nyingine kubwa, hatuna wasiwasi na safari yetu ya kuhamia Dodoma,” alisema.
Pamoja na hayo aliipongeza TALGWU kujikita katika kuweka vitega uchumi hususan majengo yaliyopo karibu na uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Wakati umefika kwa vyama vya wafanyakazi kuwa na vitega uchumi ili kuongeza mapato yake bila kutegemea makato ya asilimia mbili za mfanyakazi pekee,” alisema.
Katibu Mkuu wa TALGWU, Sudi Madega alisema wajumbe wa mkutano huo wanatoka mikoa 25 na kutaka kufanyika kwa kampeni za uadilifu bila kuchafuana ili kuwapata viongozi wazuri.