RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameongoza mamia ya wananchi katika maziko ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Pili na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aboud Jumbe Mwinyi yaliyofanyika nyumbani kwake Migombani Unguja.

Mwili wa marehemu uliwasili mapema asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amaan Karume, na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo ulifikishwa nyumbani kwake kabla ya kupelekwa katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Unguja kwa ibada.
Ibada ya kumswalia marehemu ilifanyika katika msikiti huo, ambao ujenzi wake kwa kiasi kikubwa mchango wake umetokana na Jumbe mwaka 1982. Sala ya maiti iliongozwa na Mufti wa Zanzibar, Shehe Saleh Kabi ambaye alimtaja Jumbe kuwa kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha amani na utulivu kwa kujenga uvumilivu wa kisiasa.
“Waislamu tunapaswa kuiga mfano wa Alhaji Jumbe katika kuimarisha umoja na kujenga tabia ya kuvumiliana na kuomba msamaha kwa pale anapowakosea watu,” alisema.
Safari ya mwisho ya Mzee Jumbe, ilianza nyumbani kwake Migombani ambapo alizikwa kwa heshima zote za Serikali zote mbili, ambazo alizitumikia katika kipindi kirefu cha uhai wake. Dk Shein aliongoza kuweka udongo katika kaburi la marehemu, ambalo lipo karibu na makaburi mengine manne ya watoto wake, waliozikwa jirani na eneo hilo.
Alifuatiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadaye Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa. Wengine waliopata fursa ya kuweka udongo katika kaburi la marehemu ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Viongozi wengine ni Jaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid.
Walikuwepo pia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka.
Dua ya kumuombea marehemu ilisomwa na Shehe Mohd Kassim kutoka katika Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana. Msemaji wa familia, Mustafa Aboud Jumbe alizishukuru serikali zote mbili kwa kumhudumia katika kipindi chote, ikiwemo matibabu ya nje ya nchi na ya ndani.
“Tunazishukuru Serikali zote mbili kwa kumhudumia mzee katika kipindi chote cha ugonjwa wake kwa kumsafirisha nje ya nchi na kupata matibabu ya ndani,” alisema Jumbe.
Baadhi ya viongozi walimuelezea Mzee Jumbe kuwa ni nguzo imara ya Chama Cha Mapinduzi, kwa kuunda chama ambacho nguvu zake zimekuwa imara hadi leo kwa kushinda katika chaguzi mbalimbali katika mfumo wa vyama vingi.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mohamed Ramia alimtaja Jumbe kama kiongozi aliyekuwa akiwaamini vijana kushika nafasi za uongozi, ikiwemo yeye kumpa nafasi hiyo nyeti.
Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Dk Salim Ahmed Salim alimtaja Mzee Jumbe kuwa ni kiongozi hodari, ambaye alimsaidia wakati aliposhika madaraka na nyadhifa mbalimbali za uongozi. Dk Salim alisema alianza kukutana na Jumbe wakati akiwa mwalimu wake katika Shule ya Sekondari Lumumba katika miaka ya 1958.
Aboud Talib Aboud ni mwanafunzi wa Mzee Aboud Jumbe, ambaye alipata kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi yake na kujiuzulu na anamtaja Jumbe kuwa kiongozi na mwanasiasa aliyepevuka akiwa na muono wa mbali.
Miongoni mwa wanafunzi wake wa darasani ni Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alimteua kuwa msaidizi wake katika Ofisi ya Rais hadi kuwa Waziri wa Elimu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miaka ya 1983.
Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Ali Karume anamtaja Mzee Jumbe kuwa ni sawa na baba yake mzazi, ambaye alichukuwa nafasi kubwa ya kumfariji baada ya baba yake aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kuuawa.
Ramadhan Abdalla Shaaban ni Waziri aliyefanya kazi na Alhaji Jumbe akiwa Waziri wa Biashara na Viwanda katika miaka ya 1983, ambaye anamtaja kuwa kiongozi aliyefanya kazi naye vizuri kwa ufanisi mkubwa.
Aliutaja mchango wa Jumbe kuwa ni pamoja na kuanzisha Baraza la Wawakilishi katika mwaka 1979 pamoja na Katiba ya mwaka 1984, kwa kutenganisha mihimili miwili ya dola kwa ajili ya kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Ali Abdallah Uchupa alisema alifanya kazi karibu na hayati Jumbe wakati akiwa katika chama hicho.