WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema itafuatilia malalamiko kuhusu kitendo cha kufungwa wakati wa usiku kwa baadhi ya vituo vikubwa vya Polisi jijini Dar es Salaam, hatua inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Masauni alisema wizara hiyo itafanya ukaguzi wa kina ili kubaini kama vipo vituo vya Polisi, vinavyopaswa kuwa wazi wakati wa usiku, lakini badala yake vinafungwa na kufanya wananchi kushindwa kupata huduma. Masauni alisema vituo vya Polisi vinapaswa kufanya kazi muda wote hata wakati wa usiku, isipokuwa Vituo Daraja C pekee, ndivyo vinapaswa kufungwa nyakati za usiku.
Alisema vituo vyenye Daraja A na B, vinapaswa kufanya kazi muda wote, hivyo endapo kuna vituo vyenye madaraja hayo vinafungwa vinakwenda kinyume hivyo atafuatilia ili kubaini vituo hivyo.
Vituo vya Polisi vya Daraja A na Daraja B ni vile ambavyo vinajengwa katika Makao Makuu ya Wilaya na Mikoa ya Kipolisi na katika miji inayokua, wakati Vituo vya Daraja C ni vituo vidogo maarufu kama Polisi Posti.
Katika kukabiliana na vitendo vya uvamizi katika vituo vya Polisi na kupora silaha, Jeshi la Polisi lilitangaza kufungwa kwa vituo vidogo vya Polisi ifikapo saa 12 jioni.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini vituo vikubwa vya Daraja B kikiwemo Kituo cha Polisi cha Tabata jijini Dar es Salaam, vimekuwa vikifungwa usiku na wananchi kulazimishwa kueleza shida zao nje ya kituo na baadaye kuamriwa kurejea asubuhi bila kupewa msaada.
Akizungumzia suala hilo, Masauni alisema; “Taratibu zinafahamika kwa madaraja A na B kufanya kazi muda wote na Daraja C pekee ndivyo vinapaswa kufungwa, nitafuatilia ili kubaini vituo hivyo ili tuweze kuchukua hatua.”