Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
SERIKALI imesema kuna watu wanamiliki viwanja kati ya 700 hadi 10,000 na vimepatiwa hati, lakini wamevishikilia bila kuviuza, wakisubiri kupanda thamani kwa ardhi ya maeneo yao na kuwauzia wananchi, hivyo serikali imewataka kuviendeleza au kuviuza, la sivyo itavitaifisha.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka watu wote walionunua mashamba na kupima viwanja na kupatiwa hati kwa lengo la kuuza viwanja hivyo, wafanye hivyo ndani ya siku 90 vinginevyo serikali itawafutia hati hizo.

Lukuvi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wamiliki wa kampuni binafsi za mipango na upimaji miji, aliokutana nao kwa lengo la kuwataka waanze kazi ya kupanga miji na kupima maeneo nchini ambayo halmashauri zitayatangaza kisheria kuwa miji.
“Wapo watu na ninawafahamu ambao walinunua viwanja na mashamba na ninyi mkawapimia na kuja kuchukua hati kwa majina yao halafu viwanja hivyo hawaviuzi na wamefungua masijala majumbani mwao kwa lengo la kusubiri bei zipande wawauzie wananchi… nawapa miezi mitatu wawe wameuza viwanja hivyo vinginevyo tutawafutia hati zao,” alisema Lukuvi.
Lukuvi alisema anawajua watu hao na yupo ambaye kwa siku moja, alichukua hati za viwanja 700 peke yake wizarani hapo, lakini hajaviuza hadi leo, hivyo aliwataka wamiliki hao ambao wengine wana hati hadi 10,000 wanasubiri hadi miaka 10 ndio waviuze.
Alisema wamiliki wa viwanja hivyo, watangaze kupitia magazeti juu ya kuuza viwanja hivyo, vinginevyo watapitisha msako na wakibainika bado wamehifadhi viwanja hivyo moto utawawakia. Lukuvi alisema kama wamiliki hao, wanavitaka viwanja hivyo, basi waviendeleze na wasipofanya hivyo watavitaifisha viwanja hivyo kwa kushindwa kuviendeleza.
Katika kutafuta maoni ya kisheria juu ya uamuzi huo wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, gazeti hili lilitafuta baadhi ya wanasheria na kusema kuwa uamuzi huo wa serikali ni wawazi, kwani ardhi ni mali ya serikali na ina mamlaka kisheria kutoa maamuzi yoyote.
“Watanzania wengi tumejisahau sana juu ya nani hasa mmiliki wa ardhi, ardhi ni mali ya serikali, ndio maana inakupa hati na wakati wowote kama imekutaka uiendeleze hati hiyo iliyokupa na wewe hujafanya hivyo inaweza kuichukua na kukufidia kama kuna gharama zako,” alisema Wakili Emmanuel Makene.
Aidha, Lukuvi alisema katika kukabiliana na wahalifu wa namna hiyo na kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, wameamua kuzipa idhini kampuni binafsi za mipango miji na upimaji ardhi kufanya kazi hiyo.
Alisema nchini kwa sasa kuna kampuni za kupanga 33 na kupima 58, ambazo zimesajiliwa kisheria hivyo zisambae nchini kote kufanya kazi ili kutimiza lengo lililokusudiwa la serikali la kupima na kutoa hati kwa watu wengi zaidi.
Alisema serikali ina uhaba wa watumishi hasa katika sekta ya ardhi, upande wa mipango na upimaji, hivyo kuwapa kazi hiyo sekta binafsi kwani wao watakuwa waaminifu na watafanya kazi kwa wakati.
Alisema awali kazi ya upangaji na upimaji ilikuwa inafanywa na idara za ardhi za wilaya na kampuni binafsi chache, zilizokuwa na watu wao na kutumia ujanja wao walikuwa wakipenya na kufanya kazi hizo lakini sasa kazi hiyo imerasimishwa rasmi kwa sekta binafsi ili kazi ifanyike kwa ufanisi.
Aidha, amesema licha ya Tanzania kuwa na ardhi kubwa, lakini hadi sasa ni hati milioni 1.7 tu ndio zimetolewa jambo linalowafanya watu wengi kuishi katika maeneo ambayo hayajapimwa na serikali imejipanga kwa mwaka huu kutoa hati 400,000 za viwanja na mashamba hivyo ameamua kushirikisha sekta binafsi katika kufikia lengo hilo.
Katika hatua nyingine, Lukuvi amekabidhi fomu za kupatiwa hati mbadala kwa wananchi 446 wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ambao viwanja vyao viliuzwa mara mbili na maofisa ardhi wa wizara na halmashauri ambao walikuwa si waaminifu.
Lukuvi alisema Wizara yake imetenga jumla ya viwanja 600 kwa ajili ya kuwafidia watu hao na kuwataka kujitokeza na vielelezo vyao vyote ili wafidiwe viwanja hivyo.