Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
UKAGUZI uliofanywa katika shule za msingi 6,831 zilizokaguliwa mwaka 2015/16 umebaini kuwa, wanafunzi 10,273 katika shule 515 nchini hawajui kusoma wala kuandika.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Uthibiti Ubora wa Shule katika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Marystella Wasena jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia mikakati ya kukagua na kusimamia utekelezaji wa ufundishaji wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwenye shule za awali na msingi.

Alisema miongoni mwa wanafunzi hao 10,273, wasichana ni 5,263 na wavulana ni 5,010, huku tathmini ikibainisha kuwa sababu mojawapo ya tatizo hilo ni wanafunzi wenyewe kushindwa kumudu kujifunza. Pia zipo sababu zilizotokana na watekelezaji wa mtaala wakiwemo walimu kukosa umahiri wa kufundisha KKK.
Kutokana na hali hiyo, alisema idara inaendelea na mipango ya kuwajengea uwezo wathibiti ubora wa shule ili wapate umahiri huo shuleni.
Alisema katika awamu ya kwanza, idara kupitia mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) imeshawawezesha wathibiti ubora wa shule 1,469 kupitia mafunzo elekezi yaliyofanyika Mei mwaka huu katika vyuo vya ualimu vya Patandi (Arusha), Butimba (Mwanza), Mtwara, Morogoro na Kleruu (Iringa).
Alisema kupitia mafunzo hayo yaliyofanyika Mei, idara iliazimia kuanzisha uthibiti ubora wa ndani ya shule kwa kuhakikisha kila kanda na kila wilaya inateua shule mbili za mfano zikiwemo shule za serikali na binafsi ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa.
Naye Mthibiti Ubora wa Shule Elimu ya Awali na Msingi, Hawa Selemani alisema shule binafsi zinafanikiwa katika eneo hilo kwa sababu zinachukua wanafunzi wachache kwa kila darasa tofauti na za serikali ambazo zinalenga kutoa huduma.