Mkuu wa Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo, Raun Swanepoel   akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu kampuni hiyo kugawa faida kwa watumiaji wake wa huduma kwa njia ya simu ambapo ni kiasi cha bilioni 5.6 kwa watumiaji wa Tigo pesa,kushoto kwake ni Meneja chapa ,William Mpinga katika mkutano uliofanyika mwishoni wa wiki iliyopita.



Dar es Salaam,   Agosti 09, 2016 -Kampuni inayoongoza kwa mtindo wa maisha ya
kidijitali, Tigo imetangaza tena gawio la robo mwaka la shilingi bilioni 5.6 kwa
watumiaji wa Tigo Pesa  ikiwa ni mara ya tisa kwa kampuni hiyo ya simu
kugawa faida hiyo kwa watumiaji wake wa huduma ya fedha kwa njia ya simu.

 Akizungumza
katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Huduma
za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo, Raun Swanepoel alisema kwa ujumla
kampuni hiyo  imeshalipa watumiaji wake wa huduma za fedha kwa njia ya
simu  jumla ya shilingi bilioni 46.2 ikiwa ni malipo ya  robo mwaka
tangu  kuzinduliwa kwa huduma hiyo Julai 2014.

 Swanepoel
alisema kwamba katika robo ya pili ya mwaka huu kiwango cha faida
kilipanda  na kufikia asilimia 8 kulikosababishwa na  kuongezeka kwa
kiwango cha hisa katika mabenki mbalimbali ya biashara.

 “Faida hii ya
hisa inalipwa  wateja binafsi, mawakala wa reja reja na washirika wengine
wa kibiashara wa Tigo ambao kila mmoja anapokea malipo yake kulingana na
thamani ya fedha zilizowekwa kielektroniki ndani ya pochi zao za Tigo Pesa,”
alisema Swanepoel.

Swanepoel aliongeza:
“Kusema kweli tunafurahi kutangaza ongezeko hili la faida katika gawio la mara
ya tisa mfululizo. Hii inaonesha  jinsi tulivyojikita katika
kuwawezesha wateja wetu kufikia  huduma za kifedha  pamoja na nchi
zima kwa ujumla  kupitia huduma za Tigo Pesa”.

Alibainisha ongezeko la
faida la Tigo, kuboreshwa kwa mazingira ya soko na kuongezeka kwa idadi ya
watumiaji wa Tigo Pesa kama moja ya kichocheo kilichosababisha kuongezeka kwa
faida hususani kwa upande wa wafanyabiashara. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao
mkubwa wa wafanyabiashara  zaidi ya 50,000.

 Swanepoel
alisema kuwa kama ilivyokuwa hapo awali gawio kwa wateja  linakokotolewa
kwa kuangalia wastani wa salio la kila siku la mteja la Tigo Pesa katika pochi
yake ya simu na kuongeza kuwa mpango huu wa kugawa faida umeainishwa katika
kanuni za Benki Kuu iliyotolewa February 2014.


 Mwaka 2014 Tigo
Tanzania  ilikuwa kampuni ya kwanza ya simu duniani   kugawa faida iliyozalishwa na fedha za simu
zilizopo katika Akaunti ya Udhamini kwa kipindi cha robo mwaka kwa wateja wake.


 Mwisho