Serikali ya Sudan Kusini imewaajiri watoto wavulana kama wanajeshi wakati huu inapojiandaa kwa mzozo mpya, kwa mujibu wa shirika la Associated Press.
Mwanasiasa mmoja mwenye ushawishi anaripotiwa kuongoza shughuli ya kuwaajiri watoto hao, wengine wakitajwa kuwa na umri wa hadi miaka 12 kutoka kijiji kimoja nchini humo.
Nyaraka zinaonyesha kuwa shughuli ya kuwaajiri watoto hao, ilifanyika muda mfupi baada ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kuidhinisha azimio wiki moja iliyopita la kutuma wanajeshi 4000 kwenda Sudan Kusini, kuwalinda raia baada ya kuzuka mapigano mapya katika mji mkuu Juba mwezi uliopita.
Mapigano hayo yamekuwa kati ya vikosi watiifu kwa rais Salva Kiir na vile vya makamu wake aliyefutwa kazi Riek Machar ambaye tayari ameikimbia nchi hiyo.

Zaidi ya watu 100,000 walikimbia makwao baada ya mapigano ya mwezi JulaiImage copyrightAFP
Image captionZaidi ya watu 100,000 walikimbia makwao baada ya mapigano ya mwezi Julai

Shirika la kuwahudumia watoto la umoja wa Mataifa UNICEF linasema kuwa zaidi ya watoto 650 wameajiriwa na makundi yaliyojihami nchini Sudan Kusini tangu mwanzo wa mwaka huu.
UNICEF sasa ina hofu kuwa mzozo huo mpya huenda ukahatarisha maisha ya maelfu ya watoo na kutaka shughuli hiyo ya kuwajiri watoto isitishwe mara moja.
Pia inakadiriwa kuwa watoto 16,000 wameingizwa kwa makundi yaliyojihamia na pia jeshini tangu mzozo nchini Sudan kusini uanze mwezi Disemba mwaka 2013.
Akiongea baada ya kufanya ziara katika maeneo ya Bentiu na Juba nchini Sudan Kusini, mkurugenzi mkuu wa UNICEF Justin Forsyth, alisema kuwa kuna hofu kuwa huenda watoto zaidi wakaingizwa jeshini.