WATU watatu wameuawa katika matukio tofauti ya uhalifu, yaliyotokea Dar es Salaam, likiwemo la mtu aliyelipua bomu akitishia kuwaua walinzi shirikishi.
Katika tukio lingine; watuhumiwa wawili wa ujambazi wameuawa katika maeneo ya Chiwanda Tandika, wakati wa majibizano ya risasi ya ana kwa ana na polisi wa kikosi maalumu cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Polisi kanda hiyo inamshikilia mfanyabiashara, Yoram Mbyellah (42), mkazi wa Mburahati kwa kupatikana akiuza fulana zenye maneno yanayodaiwa ni ya uchochezi zikiwa na alama ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro.
Katika tukio la bomu, Kamanda Sirro alisema jana saa 9:45 alfajiri katika maeneo ya Mabibo Loyola, walinzi shirikishi wa eneo hilo wakiwa kazini, waliwaona watu wanne wakiwa wanatembea na kuwatilia mashaka.
“Baada ya kuwatilia mashaka waliwasimamisha ili waweze kuwahoji, lakini katika mahojiano watuhumiwa wengine walikimbia na mtuhumiwa mmoja mwanaume asiyefahamika anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 na 25 alikamatwa.”
Alisema baada ya kukamatwa, mtuhumiwa huyo alianza kuwatisha kuwa atawaua huku akitamka maneno ya Kiislam akisema “Taqbir” na “Allah Aqbar” na ghafla mtuhumiwa huyo, aliingiza mkono mfukoni na kutoa kitambaa cha kufuta jasho na kukitupa chini ambapo bomu lililipuka.
“Baada ya walinzi shirikishi kuona hivyo walikimbia na mtu huyo kuanza kukimbia huku akiwa na begi mgongoni lakini mmoja kati ya walinzi hao alimpiga na rungu kichwani eneo la kisogoni,” alisema.
Kamanda Sirro alisema pamoja na mtuhumiwa huyo kupigwa rungu kichwani, aliendelea kukimbia na alitupa begi lake chini na walinzi waliendelea kumkimbiza na kufanikiwa kumkamata ambapo wananchi walijitokeza na kumpiga hadi kufa na kisha kumchoma moto.
Alisema askari polisi baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio, ambapo ulifanyika upekuzi katika begi hilo na kukutwa magazini 10 za bunduki aina ya SMG zikiwa na jumla ya risasi 300.
“Askari wapo eneo la tukio wakifanya upekuzi na msako mkali katika nyumba mbalimbali kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao inasadikiwa walikimbia kwenye tukio lakini bado wapo eneo hilo,” alisema.
Katika tukio la pili, Kamanda Sirro alisema watuhumiwa wawili wa ujambazi waliuawa juzi saa 3.30 usiku katika maeneo ya Chiwanda Tandika wakati wa majibizano ya risasi ya ana kwa ana na polisi wa kikosi maalumu cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha cha kanda hiyo.
Kamanda Sirro alisema tukio hilo lilitokea katika nyumba namba 8 ambapo askari walipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna kundi la majambazi wanataka kuvamia nyumba hiyo.
“Mara baada ya kupokea taarifa hizo askari walifika eneo la nyumba hiyo kabla watuhumiwa hao hawajaanza kupora… watuhumiwa hao walikuwa watano na pikipiki mbili ambazo hazikusomeka namba,” alisema.
Alisema baada ya watuhumiwa hao kugundua kwamba wanafuatiliwa walianza kuwafyatulia risasi askari, ambazo hazikuleta madhara na ndipo askari walijibu mapigo na kufanikiwa kuwapiga risasi watuhumiwa wawili wanaume wenye umri kati ya miaka 25 na 30 ambao walikufa papo hapo na wengine watatu walitoroka.
Alisema katika upekuzi, mmoja wa watuhumiwa hao alikutwa na bastola moja aina ya Browning ikiwa na risasi sita namba zake zikiwa zimefutwa na jitihada za kuwatafuta watuhumiwa waliokimbia zinaendelea.
Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalumu inamshikilia mfanyabiashara Mbyellah, mkazi wa Mburahati kwa kupatikana akiuza fulana zenye maneno yanayodaiwa ni ya uchochezi zikiwa na alama ya Chama cha Chadema.
Kamanda Sirro alisema juzi saa 12 jioni polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba katika maeneo ya mtaa wa Ufipa Kinondoni, kuna duka linauza fulana za rangi mbalimbali zenye maneno ya uchochezi yaliyoandikwa ‘Tujipange Tukatae Udikteta Uchwara’.
Alisema polisi walifika dukani kwa mtuhumiwa huyo na kumkamata akiuza fulana hizo zenye maandishi ya ‘Tujipange Tukatae Udikteta Uchwara’ na zilikutwa fulana za rangi nyeupe 28. Aidha alisema kulikuwa na fulana za rangi nyekundu 18 zenye maneno “UKUTA”, fulana sita za kakhi zenye maneno “UKUTA” na fulana za rangi nyeusi 23 zenye maneno “UKUTA” .
Alisema mfanyabiashara huyo anaendelea kuhojiwa na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani. Katika tukio jingine, Kamanda Sirro alisema wanamshikilia Omary Gilliad (35) kwa wizi wa gari namba T 612 AUJ aina ya Toyota Hiace, mali ya Kaisari Yusuf (26), mkazi wa Sinza lililoibwa likiwa limeegeshwa nyumbani kwa mlalamikaji.
Alisema baada ya mtuhumiwa kuiba gari hilo Juni 25, mwaka huu, alilipeleka mafichoni Masasi Mjini mkoani Mtwara, ambapo Kikosi cha Kupambana na Wizi wa Magari cha Polisi Kanda Maalumu kilifanya ufuatiliaji na kulikamata gari hilo pamoja na mtuhumiwa ambaye anatarajiwa kufikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.