Rais John Magufuli akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu)
SERIKALI imeridhia rasmi utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Kabaale katika wilaya ya Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, nchini.
Uamuzi huo umefikiwa katika Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika jana, Ikulu, Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Rais John Magufuli.

Taarifa ya hatua hiyo ya serikali kuridhia rasmi ujenzi wa mradi huo ilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kikao hicho.
Majaliwa alisema ujenzi wa mradi huo utakaoanza wakati wowote kuanzia sasa, unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujenzi wa bomba hilo unatarajiwa kugharimu dola za Marekani bilioni 3.5 na kati ya fedha hizo dola bilioni tatu zitatumika kujenga bomba upande wa Tanzania.
Mradi huo mkubwa utatekelezwa kwa ubia wa ujenzi na uendeshaji kwa kushirikisha kampuni za Total ya Ufaransa, CNOOC ya China, Tullow ya Uingereza na Serikali mbili za Tanzania na Uganda.
Majaliwa alisema kuwa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1,443 linatarajiwa kusafirisha mapipa ya mafuta ghafi 200,000 kwa siku na kila pipa litaliingizia taifa dola za Marekani 12.2.