HOSPITALI ya kisasa ya kufundishia wataalamu wa afya na kutoa huduma ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyopo eneo la kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kufunguliwa rasmi na kuanza kutoa huduma Januari mwakani.

Hospitali hiyo iliyojengwa kisasa kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), itakuwa ya kwanza kutumia mfumo wa teknolojia ya sampuli hewa, unaochukua vipimo kwa mtambo maalumu na kuwasilisha majibu kwa njia ya mtandao na itakuwa na wadi ya watu mashuhuri akiwemo Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara maalumu katika jengo hilo lililokamilika ujenzi wake tangu Agosti mwaka huu, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Ephata Kaaya, alisema hospitali hiyo, itatoa tiba ya magonjwa yakiwemo sugu kama vile moyo, saratani na figo.
Alisema hospitali hiyo, imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya dijitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalumu kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake, mashine maalumu za kupima na kutibu meno, koo, masikio na pua.
“Pia tumefunga mtambo wa kisasa zaidi wa sampuli hewa uliopo katika kila idara na kuunganishwa na maabara ambao kazi yake ni kusafirisha vipimo na kupeleka sehemu mbalimbali na majibu ya vipimo hivyo huwasilishwa sehemu husika kwa njia ya mtandao,” alisema.
Alisema mtambo huo, unasaidia kupunguza tatizo la msongamano katika chumba cha maabara, unaongeza ufanisi na usahihi wa vipimo lakini pia hupunguza muda na kuepusha mkanganyiko wa vipimo. Profesa Kaaya alisema hospitali hiyo pia itatoa huduma za kufundishia, kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na tafiti za fani za afya.
“Lakini pia tuna vyumba maalumu 12 kwa ajili ya wagonjwa wenye magonjwa ambukizi kama vile ebola, kipindupindu na kifua kikuu,” alisema.
Alisema jengo la hospitali hiyo lina ghorofa tisa ambazo zinajumuisha vyumba 13 vya upasuaji kikiwemo chumba kimoja cha upasuaji kwa wagonjwa wa dharura, maabara za kisasa, vyumba vya wagonjwa mahtuti na kusafisha figo, wodi za kujifungulia, chumba cha kuhifadhi maiti na vyumba vya kufundishia.
Aidha alisema katika eneo la wodi zipo wodi 12 za wagonjwa mashuhuri vikiwemo vyumba viwili vyenye mitambo ya kisasa ya kufuatilia hali ya mgonjwa vya viongozi wenye hadhi ya juu akiwemo Rais.
Profesa Kaaya, alisema ujenzi wa hospitali hiyo uliogharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 94.5 katika eneo hilo la Mloganzila lenye ukubwa wa ekari 3,800, ulianza tangu mwaka 2014 kupitia mkopo wenye riba nafuu ambao malipo yake yataanza kulipwa baada ya miaka 15 kwa kipindi cha miaka 25.
Kwa mujibu wa Profesa Kaaya, hospitali hiyo itakayokuwa pia ya rufaa, itasaidia kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wenye magonjwa sugu kwenda nje ya nchi kutibiwa kwani itatoa tiba na vipimo vya magonjwa mengi sugu yanayosumbua Watanzania.