Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Speak Up for Africa, limemtunukia tuzo Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kutokana na uongozi wa kisiasa na utetezi wake kwa makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.

Utoaji wa tuzo hiyo, umekwenda sambamba na hafla ya miaka mitano ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo, iliyofanyika juzi jijini New York, Marekani, ikiambatana na uhamasishaji uchangiaji wa shughuli za taasisi hiyo.
Mchango ambao umetambuliwa na taasisi hiyo wakati ikifanya kazi na Kikwete, ni katika maeneo ya upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto, udhibiti wa malaria kupitia kampeni ya malaria haikubaliki, usambazaji wa vyandarua vyenye viuatilifu, kampeni ya lishe bora, na ya chanjo kwa watoto.
Taasisi hiyo kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Kate Campana, pia imemtambua Kikwete amekuwa mstari wa mbele kulisemea Bara la Afrika kila mara alipopata fursa hiyo akiwa madarakani na baada ya kustaafu.