BARAZA Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limetangaza kumfukuza uanachama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Amefukuzwa kwa kile kilichoelezwa kuwa amekwenda kinyume na katiba ya chama na kufanya uasi kwa wanachama.

Akisoma uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa habari katika ofisi ya chama hicho iliyopo Vuga mjini Zanzibar, Mjumbe wa Baraza hilo, Katani Ahmed Katani, alisema Baraza Kuu hilo limechukua uamuzi huo chini ya Kifungu cha Katiba Ibara ya 10 (1) (c) ambapo wajumbe wote wapatao 43 walipiga kura na kukubaliana na uamuzi huo.
Katani alisema baraza hilo limemtia hatiani Profesa Lipumba kwa kitendo chake cha Septemba 24 mwaka huu, kuvamia ofisi ya chama akiwa na kikundi cha watu waliowaita wahuni na kuwapiga walinzi huku akisababisha uharibifu mkubwa wa mali za chama.
Aidha alisema baraza hilo limesikitishwa na vitendo vya dharau vya Profesa Lipumba kwa kuwa katika barua ya tarehe 24 Septemba mwaka huu, alitakiwa kufika jana katika kikao kuhojiwa, lakini alikataa.
Katani alisema hiyo ndiyo adhabu ya mwisho kwa Profesa Lipumba, ambaye hivi karibuni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, bado Lipumba alikuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.
Alisema kutolewa katika vikao halali vya baraza kuu la uongozi ambalo ndilo lenye uwezo kwa mujibu wa katiba kuwafukuza viongozi wa ngazi za juu akiwemo mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu mkuu.
Awali katika kikao hicho, Baraza hilo lilipinga vitendo vya matamshi ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Mutungi vya kuingilia mambo ya ndani ya chama hicho ambayo yanakwenda kinyume na kazi yake. Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa CUF kilifanyika chini ya mwenyekiti, Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad.
Wakati hayo yakijiri Visiwani, kwa upande wa Bara, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watuhumiwa 22 wanaodaiwa ni wafuasi wa CUF kwa tuhuma za kupatikana na silaha za jadi za kufanyia uhalifu, sambamba na kutaka kuchoma moto makao makuu ya ofisi ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema Septemba 25 mwaka huu huko Mwananyamala, polisi iliwakamata watuhumiwa hao wakiwa na zana za kufanyia uhalifu yakiwemo mapanga na majambia.
“Watuhumiwa hawa pia walikamatwa wakiwa na visu vitano pamoja na chupa 10 za kupulizia (spray) zikiwa kwenye boksi zenye maandishi ya Kichina. Watuhumiwa hao walipanda gari la abiria aina ya Coaster yenye namba za usajili T 857 CHE inayopita njia ya Buguruni- Mwananyamala,” alisema.
Alisema watuhumiwa hao ambao wanashikiliwa kwa mahojiano, walikamatwa baada ya askari kupata taarifa kwamba wamekuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya fujo kwenye ofisi hiyo pamoja na kuichoma moto.
“Watuhumiwa hao walipohojiwa zaidi walieleza kuwa wao ni wanachama wa CUF kutoka Unguja kwenye matawi mbalimbali na wamekuja kwa ajili ya kazi maalumu na wapo katika kitengo cha ulinzi na kueleza kua wapo zaidi ya watu 100,” alisema.
Alisema, “Katika mahojiano zaidi walieleza kuwa wamekuja jijini Dar es Salaam kwa maelekezo ya kiongozi wao wa CUF, Nassoro Mazrui ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF ambaye aliwaamuru kuungana na walinzi wenzao wengine waliopo ofisi za chama hicho katika makao yao makuu ya CUF Buguruni”.
Sirro aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Saidi Mohamed Zaharani aliyekamatwa na boksi la ‘spray’, Hamis Hamisi, Mohisini Ally na Masoud Igasa Fumu ambao walikamatwa na visu, Juma Omary, Mbaruku Hamisi, Juma Haji Mwanga, Hamisi Nassoro Hemedi, Mohamedi Omary Mohamed, Nassoro Mohamed Ally na wenzao 12.