WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameitaka Bodi mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kupangua Menejimenti na wafanyakazi waliomo katika shirika hilo kwa kuwa waliopo hawajamridhisha.
Alisema hajaona mabadiliko yoyote waliyoyafanya Menejimenti na wafanyakazi wa kampuni hiyo na kuagiza Bodi hiyo kufanya mabadiliko katika muda wa miezi mitatu kwa kubadilisha wote au kuacha wachache na kuchukua wapya.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na Bodi hiyo yenye wajumbe sita wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Emmanuel Korosso na Mkurugenzi wa ATCL, Ladislaus Matindi walioteuliwa na Rais Dk John Magufuli Septemba 15, mwaka huu.
Alisema mategemeo ya serikali kwa shirika hilo ni kuhakikisha wanaboresha mfumo wa biashara kutoka wa zamani kwenda wa kisasa kutokana na usafiri wa anga kuwa na ushindani mkubwa kibiashara.
‘’Tutakuwa na Mikataba ya Ufanisi wa Kazi kati yangu na Mwenyekiti wa Bodi, Katibu Mkuu, Mtendaji Mkuu pamoja na watendaji na wafanyakazi wote akiwemo rubani, injinia na mkata tiketi. Mkataba huu utakuwa wa miezi sita na kama kutakuwa na mtu ameshindwa kufanya kazi kwa ufanisi ataondolewa au ajiondoe mwenyewe,’’ alisema Profesa Mbarawa.
Pia alisema watendaji katika shirika wanatakiwa kuwa waadilifu kwani kwa muda mrefu ATCL hakuna uadilifu, hali ambayo inachangia kutofanikiwa katika mikakati yake ya kibiashara.
Aliongeza kuwa Bodi hiyo inatakiwa kusimamia wafanyakazi na kwamba mtu yeyote asiye na uadilifu aondoke mapema. Hata hivyo, alisema kuwa ATCL inazaliwa upya hivyo ni lazima watendaji wawe na kasi kwani serikali yenyewe imesimamia ununuaji wa ndege mbili kwa muda mfupi na imefanikiwa.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, ubunifu katika biashara ni nyenzo muhimu na kwamba shirika hilo haliwezi kufika wanapotaka wasipokuwa wabunifu.
Aidha, aliibua madudu yaliyokuwa yakifanywa na watendaji wa shirika hilo kwamba kumekuwa na wizi wa mafuta ya ndege, abiria kusafirisha mizigo bila kulipia.
Akitoa mfano alisema abiria wa kwenda Comoro wamekuwa wakipakia mizigo mikubwa kwenye ndege ya shirika hilo bila ya kulipia na hata wakilipia mapato yanakuwa madogo, hivyo Bodi hiyo ihakikishe inayafanyia kazi suala hilo haraka. Pia alisema kuna wakati abiria ambao walikuwa wakisafiri kwa ndege hiyo, wanaambiwa siti zimejaa wakati zipo wazi.
‘’ATCL imekuwa ikikabiliwa na upotevu wa fedha, nasisitiza kuwa iwekwe mifumo imara, makini na mahiri katika kusimamia upotevu huu ili shirika letu tunalolifufua liweze kukua,’’ alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema serikali inategemea kununua ndege mbili aina ya jet mwakani baada ya ndege moja aina ya Bombardier Q 400 kutua nchini Jumanne wiki hii huku nyingine ikitarajiwa kutua Jumatatu ijayo.
Alisema Serikali inatambua changamoto ya madeni wanayodaiwa ATCL na kwamba itafanyia kazi changamoto hiyo huku ikitarajia miezi miwili ijayo kutoa maelekezo namna ya kuzipata ndege za jet.
Pia alisema kuwa nauli ya ndege hizo mbili zitakazoanza kazi karibuni, zitatajwa na kwamba zitakuwa nafuu kama ilivyo kwa ndege nyingine tofauti na taarifa zinazosambaa mitandaoni. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Korosso alisema kuwa watahakikisha wanakuwa na mikakati ya kibiashara yenye tija kwa kampuni hiyo.
‘’Tutayatekeleza maagizo tuliyopewa na Waziri kwani hayana mjadala na tunaahidi kuyafanyia kazi kwa haraka. Tunachokifanya sasa ni kulitambua kwa undani shirika hili,’’ alisema Korosso.
Wajumbe waliochaguliwa katika Bodi hiyo ni Dk Neema Munishi Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyebobea katika Menejimenti ya Kimataifa ya Utawala Bora na Ibrahim Mussa ambaye ni Mkurugenzi wa Utalii na Masoko kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Wengine ni Mhadhiri wa UDSM, Dk Omary Mbura aliyebobea katika Fani ya Biashara na Masoko, Dk Mussa Mgwatu ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Leonard Chimagu, Meneja wa Wakala wa Taifa wa Barabara (TANROADS) mkoani Dodoma.