Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando
POLISI mkoani Rukwa inawashikilia wazazi watatu, akiwemo mume na mke, kwa kuozesha watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 15 waliokuwa wakisoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Chipu katika Kata ya Kasense kwenye Manispaa ya Sumbawanga.

Aidha, mmoja wa watoto hao aliyeozeshwa kijijini humo anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano huku mwanamume wake anayedaiwa kuwa ni mtoto wa mwalimu mstaafu, aitwae Daud Kwitwa, akidaiwa kutoroka.
Msichana mwingine na mwanamume aliyeozeshwa walitoroka kijijini humo na kwenda katika kitongoji cha Malangali, Manispaa ya Sumbawanga mkoani humo ambapo wanadaiwa kufunga ndoa Agosti katika Kanisa Katoliki la Roho Mtakatifu, Jimbo la Sumbawanga, lililopo kwenye kitongoji cha Malangali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alithibitisha kukamatwa kwa wazazi hao na msichana mmoja, huku Polisi ikiendelea kumsaka msichana mwingine na mumewe. Wazazi waliokamatwa wametajwa kuwa ni Sabastian Sangu na mkewe Hilda Mizengo na mzazi mwingine wa kiume ni Misri Mwanakatwe.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule akizungumza na gazeti hili jana alisema walikamatwa Septemba 29, mwaka jana, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Chipu akiwa ameongozana na Ofisa Elimu Taaluma wa Manispaa ya Sumbawanga, Frank Sichalwe.
“Nilipata taarifa ya kuwepo kwa watoro sugu shuleni hapo hivyo nilipofika niliingia darasa la sita nikaomba daftari la mahudhurio na kuanza kuwaita wanafunzi jina baada ya jina ndipo ilipobainika kuwa kati ya wanafunzi 142 wanaosoma darasa hilo, 52 ndio waliohudhuria huku 90 wakikosekana shuleni na kudaiwa kuwa watoro sugu,” Haule alisema.
Alisema alipodadisi zaidi wanafunzi wenyewe walianza kueleza kuwa wengi wa watoro wanafanya kazi za vibarua vya kuchunga ng’ombe na kwamba wasichana wawili wameolewa kijijini humo.