Sehemu ya Kata ya Pinyinyi
WAKATI watu zaidi ya 21 wamekufa katika Kata ya Pinyinyi wilayani Ngorongoro mkoani Arusha kwa ugonjwa wa ajabu wa kutapika damu, Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Frida Mtiki hana taarifa juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo.
Mtendaji wa kata hiyo, James Mushi alibainisha kuwapo kwa ugonjwa huo wakati akisoma risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alipokwenda kutembelea kata hiyo kujionea shughuli za maendeleo, ikiwa ni ziara ya siku tano katika wilaya hiyo.

Baada ya Mushi kueleza katika risala yake juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka minne na watu 21 kupoteza maisha, ndipo mkuu wa mkoa alipomsimamisha Mganga Mkuu wa Mkoa ili kupata maelezo ya kwa nini mkoa haujachukuwa hatua.
Mganga huyo alisimama na kuueleza umma wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara kuwa hana taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo na wala mkoa hauna taarifa juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo.
Majibu hayo yalimchanganya na kumkasirisha mkuu wa mkoa na kuamua kumsimamisha Mganga wa Wilaya ya Ngorongoro (DMO), Omari Sukari kutoa majibu kama na yeye hana taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo.
Sukari alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo na kweli umeua watu 21 na amefanya jitihada na ziada kwa kupeleka sampuli Wizara ya Afya kwa wataalamu, kwani hata yeye ameshindwa kujua nini chanzo cha ugonjwa huo na kinasababishwa na kitu gani.
Mganga huyo wa wilaya alisema vipimo vya awali vilionesha kuwa ugonjwa huo husababishwa na ugonjwa wa kichocho, lakini bado wamejiuliza zaidi kwa kupeleka sampuli nyingine ya matapishi kwa wataalamu wa magonjwa ya binadamu kujua zaidi ukweli wa ugonjwa huo na majibu hayajarudi.
Baada ya majibu hayo, mkuu wa mkoa alieleza waziwazi kusikitishwa na kushangazwa majibu ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kusema kuwa haingii akilini ugonjwa ulioua watu 21 na uko zaidi ya miaka minne katika Kata ya Pinyinyi, lakini hana taarifa wakati mganga wa wilaya anayo taarifa.
Gambo alisema hiyo inaonesha wazi kuwa baadhi ya watumishi wa serikali mkoani, wanafanya kazi kwa mazoea na kushindwa kujua ama kupata taarifa za kila siku katika wilaya.
Alisema hilo hatalivumilia hata kidogo na kuwataka wakuu wa idara wa mikoani, kuwajibika kwa kupata taarifa za kila siku katika wilaya zote za Mkoa wa Arusha ili majibu ya kila kitu yapatikane na kupatiwa ufumbuzi wa kutosha.
“Hii ni aibu, ugonjwa upo kwa miaka minne na tayari umeua watu 21, lakini RMO hana taarifa, lakini DMO anayo taarifa na amefanya kazi ya ziada kutafuta chanzo cha ugonjwa huu,” alisema mkuu wa mkoa.
“Kama nisingekuja hapa ina maana huu ugonjwa usingejulikana wala kupata majibu ya kutosha na watu wangeendelea kufa, sasa nataka RMO kuhakikisha ugonjwa huo unakwisha na dawa inapatikana,” alisema Gambo.
Katika risala hiyo, wananchi wamempongeza mkuu huyo wa mkoa kwa kufika katika kata hiyo, kwani mara ya mwisho Mkuu wa Mkoa wa Arusha kutembelea kata hiyo alikuwa Mohamed Babu mwaka 2006.