Chama cha watu wenye ualibino mkoani
Mwanza, kimemuomba Rais John Pombe Magufuli, kukemea vikali vitendo vya ukatili
ikiwemo kutekwa na kuuawa kwa watu hao kama anavyokemea masuala ya rushwa na
ufisadi kwenye mikutano yake mbalimbali.


Mwenyekiti
wa chama hicho, Alfred Kapole, ametoa ombi hilo Jijini Mwanza wakati
akizungumzia juhudi zinazofanywa na chama hicho ili kuhakikisha vitendo vya utekaji,
ukataji viungo pamoja na mauaji kwa watu wenye ualibino nchini vinatokomezwa.


Amesema pamoja
na juhudi zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na
wanajamii katika kutokomeza vitendo hivyo, bado watu wenye ualibino nchini wanaishi
kwa wasiwasi mkubwa kwani wamekuwa wakiwindwa na baadhi ya watu wenye imani
potofu za kishirikina hivyo Rais Magufuli anapaswa kukemea vikali hali hiyo.


Mkoa wa
Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye rekodi zisizoridhisha za matukio ya kutekwa,
kukatwa viungo na kuuawa kwa watu wenye ualibino hapa nchini ambapo kesi tatu
kati ya kesi 27 zilizoripotiwa mahakamani zimetolewa hukumu yake na wahusika
kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa.
Bonyeza HAPA kusikiliza. Au bonyeza Play hapo chini.