MAMLAKA ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ukataji wa tiketi za mabasi na daladala kwa njia ya kielektroniki.
Hatua hiyo ina lengo la kurahisisha upatikanaji wa mapato halali ya serikali pamoja na kuwafanya madereva na makondakta, kuajiriwa rasmi na wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri.

Pia mamlaka hiyo imezindua kampeni ya usafi kwa wafanyakazi wa daladala, ambayo inawataka kubadilisha sare za madereva na makondata, ambazo walishonewa na matajiri wao.
Sasa wafanyakazi hao watashona sare zao wao wenyewe ili wawe na uhalali wa kuzimiliki na kuzifanyia usafiri wa mara kwa mara.
Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema jana kuwa mfumo huo wa tiketi za daladala kwa njia ya elektroniki, utaanza kutumika Januari mwaka kesho.
Lakini, aliongeza kuwa kuanzia Desemba mwaka huu, watafanya mpango huo kwa majaribio kwa mabasi yaendayo mikoani.
“Kwa sasa tumeanza mpango huo kwa majaribio kwa daladala za kampuni ya Christian, Desemba tutaenda kwa mabasi ya mikoani na Januari mwaka kesho, mfumo huo utaanza kwa mabasi na daladala zote,” alisema Kahatano.
Alitangaza mfumo huo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi kwa madereva, ambayo inahusisha usafi wa mwili, mavazi na mabasi uliofanyika katika stendi ya Makumbusho, Dar es Salaam. Katika kampeni hiyo, madereva na makondakta watajishonea wenyewe sare zao na sio wamiliki wa magari.
Kahatano alisema chini ya mfumo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki, utamfanya mmiliki wa basi kujua mapato yake halisi kwa siku na hivyo atawalipa wafanyakazi wake mshahara na Serikali itapata kiwango sahihi cha kodi. Kwa sasa ukataji wa tiketi za mabasi na ule wa daladala, unafanywa kwa tiketi zilizochapishwa.
Alisema kutokana na mfumo huo mpya, dereva haruhusiwi kumlipa mmiliki hesabu ya kila siku kama wanavyofanya sasa.
Badala yake, mmiliki ndiye atatakiwa kumlipa dereva na kondakta wa gari lake mshahara kila mwisho wa mwezi. Alisema ili malipo hayo yaweze kufanyika ni lazima madereva waajiriwe rasmi na walipwe chini ya mfumo wa ajira.
“Kwa hiyo dereva na mmiliki wataingia mkataba wa ajira tofauti na sasa hivi hakuna mkataba wowote kati ya tajiri na wafanyakazi wake, badala yake wanakubaliana tu kwamba hesabu ya siku ni kiasi fulani cha fedha na dereva anahangaika kukitafuta,” alisema Kahatano.
Kuhusu sare za madereva, alisema kwamba ndani ya wiki mbili madereva wa wilaya ya Kinondoni, wote wanatakiwa wawe wamebadili sare zao na kushona ambazo wamekubaliana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Awadhi Haji, alisema wao kama wasimamizi wa sheria, watahakikisha ndani ya wiki mbili madereva wote wa daladala wa wilaya ya Kinondoni, wanashona sare hizo mpya ambazo zimepitishwa na Sumatra.
Alisema kutokana na agizo hilo, hategemei kuwaona tena makondakta na madereva wachafu kwa kuwa watakuwa na sare zao binafsi ambazo watazitunza kuliko ilivyokuwa awali.
“Wale ambao watakaidi tutawakamata na kuwafikisha mahakamani.”
Mwenyekiti wa daladala wa vituo vya Simu 2000, Tegeta na Bunju, Stanley Kijave, alisema amefurahia mfumo wa sare za madereva na makondakta kumilikiwa na wao wenyewe na sio za tajiri kwa kuwa mfumo wa sare kumilikiwa na mmiliki wa gari ulisababisha wafanyakazi wa sekta hiyo kuwa wachafu.
Alitoa mfano kwamba mtu alikuwa akiacha kazi na kuingia dereva wa kondakta mwingine, sare zilizokuwepo kuendelea kutumika bila hata kuzingatia ukubwa wa kipimo.
Kuhusu kuanza kutumika kwa mfumo wa kutoza nauli kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, alisema mfumo huo utaleta ahueni kwa dereva na kondakta wa daladala kwa sababu wataingizwa kwenye mfumo wa ajira rasmi.
Alisema mfumo uliokuwepo wa dereva kumlipa mmiliki haukuwa unatenda haki kwa kuwa ni mfumo wa kinyonyaji ambao una lengo la kunufaisha wamiliki zaidi kuliko wafanyakazi. ‘Sasa mfumo unaokuja utakuwa wa mmiliki wa gari kumlipa mfanyakazi wake, sisi tumeupokea kwa mikono miwili.”
Alisema mfumo wa sasa wa hesabu za siku hautoi fursa kwa mmiliki kuingia mkataba wa ajira na dereva, bali kilichopo ni mahusiano tu lakini kwenye mfumo ambao utaanzishwa na Sumatra ni wazi kuwa ni lazima kutakuwa na mikataba inayoeleweka.
“Kwa hiyo na sisi madereva tutaingizwa kwenye mifuko ya pensheni.” Kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi cha Madereva, Shaban Mdemu alisema utaratibu wa kuwaajiri madereva kama chama wamekuwa wanaulilia na akashukuru Serikali kuja na utaratibu huo mpya.