Huduma ya kusafirisha damu na vifaa vingine vya kimatibabu kwa kutumia ndege zisizo na rubani, inazinduliwa leo nchini Rwanda.
Huduma hiyo ni ya kwanza ya aina yake duniani.
Ndege zisizo na marubani zitakuwa zikipaa moja kwa moja hadi eneo ambalo damu inahiajika nchini Rwanda, na kisha kurejea kituoni.
Badala ya kutua ndipo ziwasilishe kifurushi chenye damu, kifurushi hicho kitarushwa ardhini salama kwa kutumia mwavuli au parachuti.
Teknolojia hiyo inaleta matumaini ya kuwasilisha damu haraka na kwa njia salama ukilinganisha na awali ambayo njia ya kutegemewa pekee ilikuwa barabara, nyingi ambazo ambazo hali yake ni mbaya.

ZiplineImage copyrightZIPLINE
Image captionVifurushi vitakuwa vikirushwa ardhini kwa kutumia mwavuli au parachuti. Ndege hazitahitaji kutua.

Kampuni ya Marekani ya Zipline ndiyo itakayoendesha mradi huo.
Wanaofanya kazi katika kampuni hiyo ni wahandisi ambao awali walifanya kazi katika kampuni maarufu za kiteknolojia kama vile Space X, Google, na Lockheed Martin..
Mwanzoni, ndege hizo zitatumiwa kusafirisha damu, maji ya damu na dutu inayogandisha kioevu.
Ndege hizo zinaweza kuruka na kupaa zikiwa futi 500 (mita 152) juu ya ardhi kuzuia kugongana na ndege kubwa za kawaida zinazobeba abiria na mizigo.
Ndege hizo zitakuwa zinahudumu eneo la umbali wa hadi kilomita 150 (maili 93), ingawa zina uwezo wa kwenda umbali maradufu ya umbali huo.

Zipline
Image captionNdege hizo za Zipline zikirushwa angani kutoka kwenye kambi iliyopo karibu na mji wa Kigali

Ndege hizo zinatumia nguvu za umeme kutoka kwenye betri na hutumia teknolojia ya GPS kuziongoza kufika maeneo yanayotakikana.
Zitakuwa zikituma maeleo kwa wahudumu kwenye kambi ya ndege hizo na pia wahudumu wasimamizi wa safari za ndege Rwanda kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu.
Kwa kuanza, ndege 15 zitakuwa zikifanya kazi.
Ndege hizo, ambazo kwa kifupi zinafahamika kama 'Zip', zina uwezo wa kupitia hata kwenye upepo wa kasi ya kilomita 30 kwa saa (19mph) au mvua ndogo hali ikibidi.

Zipline
Image captionWakati wa kufanyiwa majaribio kwa teknolojia hiyo, jeshi la Rwanda lilionesha kuvutiwa

Zipline italipwa na idara ya afya ya Rwanda kwa kila safari itakayofanywa na ndege hizo.
Kampuni hiyo inasema gharama ya kila safari moja ni karibu sawa na ya kutumia pikipiki au ambiulensi.

ZiplineImage copyrightZIPLINE
Image captionWahudumu wa afya wanasema kuomba huduma ya Zipline kwa kutumia ujumbe mfupi

Ndege zisizo na rubani tayari zimetumiwa kwa shughuli za kibinadamu kwingineko Afrika, ikiwemo kusafirisha sampuli za damu na kinyesi nchini Madagascar. Aidha, kuna mradi wa Shirika la Msalaba Mwekundu unaotumiwa kufuatilia shughuli kambi ya wakimbizi Uganda.
Lakini baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanasema ndege hizo mara nyingi huwa hazifai.
"Upende usipende, ndege hizo mara nyingi hudhaniwa kuwa ndege za kutekeleza mashambulio au kufanya ujasusi," mmoja wa wahudumu waliofanya kazi DR Congo aliambia watafiti wa wakfu mmoja kutoka Uswizi.
Ingawa jeshi la Rwanda limeonekana kuvutiwa na kazi ya Zipline, waziri wa teknolojia, habari na mawasiliano Rwanda amesema hakuna mipango yoyote kwa sasa kwa jeshi kutumia teknolojia hiyo.