Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Oct 5, 2016

Kabila asifu mabadiliko bandarini Dar

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila ameyasifu mabadiliko yaliyoanza kuonekana katika Bandari ya Dar es Salaam, na kuihakikishia Tanzania kuwa nchi hiyo itaongeza kasi zaidi ya matumizi ya bandari hiyo.
Hadi sasa kwa mujibu wa Rais John Magufuli, mizigo inayopitia katika bandari hiyo kutoka na kwenda DRC imeongezeka kwa asilimia 10.6 huku biashara baina ya nchi hizo ikiongezeka kutoka Sh bilioni 23 mwaka 2009 hadi Sh bilioni 396.3 mwaka jana.

Pamoja na hayo, DRC na Tanzania zimesaini rasmi mkataba wa makubaliano ya kufanya utafiti wa mafuta katika Ziwa Tanganyika, ambayo yakibainika na kuanza kuzalishwa, yatasafirishwa kupitia bomba la mafuta linalotarajiwa kujengwa kutoka Uganda kuja nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Magufuli, Ikulu Dar es Salaam jana, Rais Kabila alisema nchi yake iko tayari kuendeleza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara uliopo baina ya nchi hizo mbili.
“DRC inatumia bandari ya Dar es Salaam kwa kiasi kikubwa kusafirisha mizigo yake, lakini nikiri kuwa miaka iliyopita tulikuwa na matatizo na bandari hii, lakini kwa kweli kwa sasa hali ni tofauti kwani kumekuwa na mabadiliko makubwa ya huduma katika bandari hii yanayotupa moyo,” alisema Rais Kabila ambaye aliwasili nchini juzi kwa ziara ya siku tatu inayomalizika leo.
Alisema kwa hali inavyoendelea katika bandari hiyo, ni wazi kuwa katika siku zijazo, itakuwa bandari bora Afrika itakayotumiwa zaidi, si tu na nchi chache za Afrika Mashariki, bali hata nchi za magharibi.
Alisema kijiografia, DRC upande wa mashariki imepakana na nchi nne ambazo ni Rwanda, Burundi, Uganda na Tanzania, lakini kati ya nchi hizo takribani asilimia 50 ya biashara za nchi ya Congo inafanya na Tanzania.
Alisema amefurahishwa na namna Serikali ya Awamu ya Tano, ilivyojipanga kuboresha zaidi huduma za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ikiwa ni pamoja na kushirikiana na bandari kavu zilizopo DRC, jambo litalorahisisha zaidi biashara kati ya nchi hizo mbili.
“Nimefurahi pia kuona mnazindua jengo hili litakalotengeneza kituo kimoja cha kutoa huduma za bandari. Nina imani biashara kati yetu na Tanzania itaongezeka… “… kwani pamoja na biashara nyingine, DRC tunazalisha shaba, miaka iliyopita tulikuwa tunazalisha tani 100,000 mpaka 150,000 za shaba lakini sasa kutokana na uwekezaji tunazalisha tani milioni moja mpaka milioni moja na nusu, hivyo nina imani tutazidi kushirikiana katika eneo hili lauchukuzi,” alisisitiza.
Akizungumzia mkataba wa mafuta uliosainiwa na mawaziri wa nchi zote mbili ambao ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Mafuta wa DRC, Ngoi Mukena, alisema mkataba huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano baina ya nchi hizo katika eneo la mafuta.
Alisema kwa sasa Afrika imeanza kugundua maeneo mengi yenye mafuta, akitoa mfano nchi yake ya DRC iliyogundua mafuta kupitia Ziwa Albert na Uganda ambayo imekamilisha mazungumzo ya ujenzi wa bomba la mafuta litakalopitia Tanga.
Pamoja na hayo, Rais Kabila pia alizungumzia suala la amani na uchaguzi nchini kwake, ambapo alisisitiza kuwa serikali yake iko tayari kuwahakikishia demokrasia wananchi wa Congo katika uchaguzi utakaofanyika ama mwaka huu au mwakani.
“Napenda nichukue nafasi hii niweke wazi na kupingana na uzushi mwingi wa vyombo vya habari kwamba hali ni mbaya DRC. Nawahakikishia wananchi wa Congo na Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwamba hali ya Congo ni salama na kuna amani,” alisema Rais Kabila aliyeingia madarakani mwaka 2001.
Alisema kwa sasa nchini humo kuna hali ya viguvugu la wasiwasi nchini humo kutokana na kukaribia kwa kipindi cha uchaguzi, hali ambayo ni ya kawaida kwa nchi yoyote.
“Serikali yangu imepanga kuitisha mazungumzo na kuzungumzia suala hili. Tunataka uchaguzi ufanyike kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, uhuru na amani,” alisema.
Hata hivyo, alikiri kuwa katika nchi hiyo kumekuwepo na tatizo la kiusalama kupitia vikundi vidogo vya waasi ambao mara kadhaa wamekuwa wakifanya mashambulizi, ikiwemo utekaji wa watu na kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuwa moja ya nchi zilizopeleka vikosi vyake kusaidia kurejesha amani nchini humo.
Kwa upande wake, Rais Magufuli alikiri kuwa hali ya bandari ya Dar es Salaam, imebadilika kutokana na juhudi kubwa ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imezifanya ikiwemo kuwaondoa watumishi wote waliochangia kuharibu mzingira ya kazi ya bandari hiyo.
“Ni kweli miaka ya nyuma hapa kulikuwa na watu waliojiona ni miungu watu, walitumia vibaya madaraka yao, walidiriki hadi kuweka fedha kwenye maboneti ya magari yao bila kujali maslahi ya Watanzania. Nakuhakikishia Mheshimiwa Rais Kabila katika Serikali ya Awamu ya Tano, mambo kama haya hayototokea kamwe,” alisisitiza.
Alisema kati ya mambo aliyozungumza na Rais huyo, wamekubaliana kuongeza ushiriki wa DRC kupitisha mizigo yake kwani hadi sasa DRC imefanikiwa kuongeza mizigo inayopitia bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 10.6.
Alisema pamoja na kuondoa tatizo la urasimu katika bandari hiyo, pia serikali imepunguza milolongo inayoweka vikwazo kwa wafanyabiashara wanaopitisha mizigo yao nchini kwa kupunguza idadi ya mizani ya kukagua mizigo na kufikia mizani tatu, zitakazokuwa katika maeneo ya Vigwaza mkoani Pwani, Manyoni mkoa wa Singida na Nyakahura mkoani Kagera.
“Lakini pia nimeambiwa TPA wamekubali kuwaondolea msamaha wafanyabiashara wa DRC kwa kuongeza muda wa kuweka mizigo yao bandarini kutoka siku 14 hadi siku 30,” alisema na kuongeza kuwa katika kuboresha mazingira ya biashara nchini, serikali pia kwenye bajeti yake ya mwaka 2016/17 imetenga jumla ya Sh trilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa itakayounganishwa kutoka Burundi kwenda Isaka ambayo pia itapunguza adha ya usafiri kwa wafanyabiashara wa DRC.
Aidha, alimuomba Rais Kabila naye afuatilie na kuwachukulia hatua wale wote wanaolalamikiwa katika kitengo cha ushuru na forodha wa upande wa DRC kwa urasimu ili kuweza kutengeneza zaidi mazingira mazuri baina ya nchi hizo mbili.
Kuhusu mkataba wa mafuta, Rais Magufuli alisema mkataba huo baina ya DRC na Tanzania, utarahisisha mafuta yatakayopatikana kwenye ziwa Tanganyika kusafirishwa kupitia bomba linalojengwa la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanzania.
Akizungumzia suala la ulinzi na usalama la DRC, Magufuli alisema katika mazungumzo yake na Rais Kabila, amemthibitishia kuwa nchini humo kuna hali ya usalama na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kufuata misingi ya demokrasia.
“Kwa sasa wako kwenye mchakato wa kujiandikisha kwenye daftari la kupigakura kwani nchi hii inatarajia kuwa na idadi ya wapigakura wapatao milioni 45 ambapo uchaguzi uliopita watu milioni 35 walijiandikisha kupigakura,” alisema.
Aidha, alisema amekubali ombi la Rais huyo la kutaka wafuatilie hali ya amani nchini humo na kubainisha kuwa kupitia nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chombo cha Siasa, Ulinzi na Usalama cha SADC (Troika), amewaagiza mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi tatu kufanya tathmini ya halisi ya usalama nchini humo.
Alisema mawaziri hao watakaokwenda DRC ni waziri wa mambo ya nje kutoka Tanzania, Angola na Msumbiji. Aidha, Rais Magufuli alisema pia katika mazungumzo yake na Rais Kabila, amemueleza nia yake ya kutaka nchi ya DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kumtaka awasilishe barua yake rasmi ili iweze kujadiliwa na wajumbe wengine wa jumuiya hiyo.
Rais Kabila alizindua jiwe la msingi la jengo la TPA, maarufu kama one stop centre, litakalotumika kwa ajili ya kutoa huduma zote za bandari na TRA. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedis Kakoko, jengo hilo lenye ghorofa 35 ndio refu zaidi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP