RAIS wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila amebainisha wazi kuwa anatamani nchi yake pamoja na ukubwa na utajiri iliyonayo, ingekuwa na amani na mshikamano kama Tanzania.

Pia Rais huyo amesisitiza kuwa nchi yake kwa sasa iko tayari kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi nyingine ikiwemo Tanzania, tofauti na zamani ambako ilijikita zaidi katika masuala ya kutafuta amani. Kabila aliyasema hayo juzi usiku wakati akizungumza kwenye dhifa ya chakula aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Alisema anavutiwa na hali halisi ya amani inayoendelea kudumu nchini Tanzania, ikiwemo jitihada za wananchi na serikali kwa ujumla katika kuitunza na kuilinda amani hiyo na kuimarisha uchumi.
“Kila nikipita katika mitaa mbalimbali ya DRC nakumbuka hali halisi ya amani iliyopo Tanzania. Nikiri tu nimekuwa nikivutiwa sana na hali ya amani na mshikamano iliyopo hapa Tanzania. DRC ni nchi kubwa na yenye utajiri, ninaiombea sana nchi yangu na yenyewe ifurahie amani hii,” alisisitiza.
Alisema anatambua kuwa hata nchi iwe kubwa na utajiri vipi, wananchi wake hawawezi kuwa na furaha kama hakuna amani.
“DRC ni nchi kubwa ina jumla ya makabila na lugha 225 nina imani na sisi tutaweza kuwa na amani na umoja kama mlionao hapa Tanzania.”
Aidha, Rais huyo, alisema amefurahi nchi yake kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kiulinzi na usalama na kindugu na Tanzania na kukiri kuwa hiyo ni mara yake kwanza kutembelea Tanzania na kuzungumzia zaidi masuala ya kiuchumi na kibiashara ambapo zamani ziara zake zilijikita zaidi kujadili masuala ya amani.
Awali, wakati akizindua jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), pamoja na kuihakikishia Tanzania kuwa nchi yake imeridhishwa na hali ya bandari ya Dar es Salaam hivyo itaendelea kupitisha mizigo yake katika bandari hiyo, pia aliomba ushirikiano wa nchi hizo katika sekta ya anga.
Alisema anatambua kuwa serikali ya awamu ya tano imenunua ndege mpya mbili na kwamba imepanga kuanza kufanya safari zake maeneo mbalimbali na kubainisha kuwa hata DRC nayo imenunua ndege mbili hivyo itakuwa vyema serikali hizo zikiunganisha nguvu zake pia katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Rais Magufuli, alimshukuru Rais Kabila kwa kukubali kwake kufanya ziara hiyo ya kibiashara nchini, ikiwa ni pamoja na kuihakikishia Tanzania kuwa mizigo ya DRC ikiwemo shaba inayozalishwa nchini humo, itasafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.