Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde
MBUNGE wa Mtera mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde (CCM) amehojiwa na Polisi kwa madai amekuwa na tabia ya kuwachochea wananchi wake, kujichukulia sheria mkononi katika mambo wasiyokubaliana nayo, jambo lililosababisha kuuawa kwa watafiti watatu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Arusha (SARI) ndani ya jimbo lake.

Pia imebainika kuwa watafiti hao, ambao waliuawa na wananchi kwa kucharangwa kwa rangwa kwa mapanga na shoka katika Kijiji cha Iringa Mvumi, walikuwa na barua ya kuwatambulisha kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwenda kwa mtendaji wa kijiji hicho.
Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Polisi Mkoa wa Dodoma, zilithibitisha kwamba mbunge huyo aliitwa jana kuhojiwa kutokana na kudaiwa huwa anashiriki kuwachochea wananchi wake, kuchukua sheria mkononi kwa mambo ambayo hawakubaliani nayo.
“Ni kweli mbunge tumemwita asubuhi na kumhoji kuhusu taarifa hizo, tunashukuru ametupa ushirikiano, na kikubwa tulichokuwa tunahitaji kutoka kwake ni hizi taarifa za yeye kuhamasisha wananchi wake kujichukulia sheria mkoanoni,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Polisi Dodoma. Mbunge akanusha kuchochea Lusinde alipoulizwa kuhusu kuhojiwa na polisi jana alikataa. “Nihojiwe kwa jambo gani? alihoji mbunge huyo.
Hata hivyo alibanwa kwamba alionekana kituo ha polisi asubuhi na kuulizwa alienda kufanya nini, alikiri kwamba alienda kituo cha polisi. “Ni kweli nilienda polisi asubuhi, lakini nilienda pale kuwaona viongozi wanaoshikiliwa na polisi, maana kuna diwani na mwenyekiti wa kijiji, hawa ni viongozi wenzangu lazima niwaone, lakini sikwenda kuhojiwa na polisi,” alisema Lusinde.
Kuhusu tuhuma za yeye kushiriki kuwachochea wananchi wake, kujichukulia sheria mkononi kwa mambo wasiyoyakubali, Lusinde alisema tangu uchaguzi mkuu wa mwaka jana uishe, hajawahi kufanya mkutano wowote kijijini hapo wala kwenda kushiriki kwenye ibada.
“Tangu uchaguzi uishe sijawahi kukanyaga kijijini hapo huo uchochezi nimeufanya saa ngapi? Aliongeza, “Kuna wataalamu wa maji na miradi mingine wanafika kijijini hapo hawajawahi kupigwa. Mimi ni mbunge nitaanzaje kuwachochea wananchi wangu? Kwa kweli huo ni uongo na uzushi dhidi yangu.”
Alitoa mwito kwa wananchi ambao wamekimbia makazi yao kurudi kijijini na kushirikiana na vyombo vya dola ili waweze kuwataja walioshiriki kwenye mauaji hayo.
“Mauaji yalifanyika mchana, ina maana waliofanya mauaji wanafahamika, wananchi warudi wawataje bila kuwaonea haya.” Akielezea tukio hilo alisema tukio la umwagaji damu kwa watu wasio na hatia ni laana, hivyo yeye kama mbunge anasubiri polisi wakishakamilisha taratibu za upelelezi, atamwomba Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Kati (DCT), Dk Dikson Chilongani ili akafanye ibada katika eneo hilo. “Ni lazima tukamlilie Mungu na kumwomba samahani kwa mauaji haya yaliyofanyika pale,” alisema mbunge huyo.
Alisema yeye binafsi hajawahi kusikia kuwepo kwa wanyonya damu katika vijiji vya jimbo lake. Watafiti walifuata taratibu Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Mkurugenzi Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Hussein Mansoor alisema watafiti hao walipitia taratibu zote za kujitambulisha kuanzia mkoani, wilayani na kwa watendaji wa vijiji na kata.
“Bahati nzuri hata kwenye gari kulikuwa na nakala ya barua yao ya kuwatambulisha iliyokuwa imetumwa na halmashauri kwenda kwa watendaji wa vijiji ambako walitakiwa kwenda kufanya kazi na hata pale walipouawa uongozi wa kijiji ulikuwa na taarifa,” alisema Dk Mansoor.
Chanzo cha polisi Dodoma pia kilikiri kuwa eneo la tukio waliokota barua kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwenda kwa mtendaji wa kijiji hicho, kuwatambulisha watafiti hao. “Hawa walifuata taratibu zote, yawezekana hatua waliyoiruka ni kwenda kujitambulisha ofisi ya kijiji na kupewa wenyeji wa kuwaongoza kufanya kazi zao, hilo tunahisi hawakulifanya,” alieleza.
Akifafanua kuhusu watafiti hao, Dk Mansoor alisema watafiti hao walikuwa wanafanya kazi chini ya mradi ujulikanao kama Tanzania Soil Information System (TANSIS) ambao unaendeshwa na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kupata ramani ya udongo nchi nzima ili kuwashauri wakulima kwa kutoa ushauri sahihi kwa kutumia taarifa za udongo za sasa.
Akielezea taratibu zinazotumiwa na wizara hiyo pindi watafiti wake wanapoenda mikoani, Dk Mansoor alisema wanaandika barua kwa mkoa na wilaya husika kuwatambulisha watafiti hao na kazi watakayoifanya na muda wa siku watakaokuwepo humo.
“Kwa hili la Chamwino, wizara tulipeleka barua mkoani na wilayani, na pia taarifa zilipelekwa na wilaya kwa watendaji wa kata na vijiji ambako walikuwa wamepangiwa kwenda kufanya kazi. “Huwa tunawashauri wawe na nakala za barua kwa kile eneo ambako wanaenda, na bahati nzuri nakala ya barua ya kwenda kwa mtendaji wa kijiji kile ambako waliuawa walikuwa nayo kwenye gari na ilidondoka katika purukushani zile na polisi wameiokota,” alisema Dk Mansoor.
Alisema utafiti waliokuwa wanaufanya watafiti hao ni muhimu kwa mkulima kwani ni utafiti huo ndio ambao unatoa fursa ya kuwashauri wakulima aina ya mbolea wanayotakiwa kutumia na kiwango cha mbolea hiyo kutokana na hali ya udongo. Katibu Tarafa awakana Hata hivyo, Katibu Tarafa ya Makang’wa, Hanifa Diemerwa alisema wakati tukio linatokea yeye alikuwa likizo hivyo hana taarifa yoyote.
Hata hivyo alipoulizwa kama ameshafuatilia kama ofisi za kijiji zilikuwa na taarifa za ujio wa watafiti hao, alijibu kuwa hakukuwa na barua yoyote ya kuwatambulisha watafiti hao.
“Mimi nimejaribu kufuatilia wanasema hakukuwa na barua, hata hivyo kama walikuwa na hiyo barua, basi walikuwa hawajafika kujitambulisha kwenye ofisi ya kijiji na kusaini kitabu cha wageni,” alisema Hanifa.