WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameanza shughuli zake za kiofisi kwa kishindo kwa kutembelea maeneo ya kutolea huduma muhimu kwa jamii yakiwemo masoko, afya na makazi baada ya kukaribishwa ofisini kwake.
Pamoja na kutoa maagizo ya mabadiliko yanayotakiwa ili kuendelea kuipokea serikali iliyoanza kuhamia Dodoma, pia amewatoa shaka watumishi watakaohamia hapa kuwa hakuna shida ya huduma za afya na maeneo ya kupata mahitaji ya msingi kama chakula na makazi.

Aidha Waziri Mkuu ambaye alitembelea maeneo ya utoaji wa huduma hizo kabla ya kuzungumza na watumishi wa Serikali wa mkoa wa Dodoma, wazee wa mkoa huo, wafanyabiashara pamoja na viongozi mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano wa Dodoma (Dodoma Convention Centre), alisema Serikali imeunda timu ya wataalamu ambao watatoa ushauri juu ya suala zima la kuhamishia makao makuu Dodoma kuhakikisha kwamba makosa yaliyofanyika Dar es Salaam hayarudiwi mkoani hapa.
“Tumeunda timu ya watu 10 ambao ni wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi wa miji mikuu, hawa wana uzoefu wa kuangalia makao Makuu ya nchi yanafananaje. Watakuja Dodoma, wapitie master plan na kisha watapita kwenye maeneo kadhaa ya mji ili waone hali halisi ikoje ndipo watupe maoni yao,” amesema.
Akizungumza kiujumla kuhusu huduma za kijamii kama elimu, umeme, maji na masoko, Waziri Mkuu amewahakikishia watumishi kwamba Serikali imeangalia kila eneo na kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha utoaji wa huduma hizo.
Amewataka watumishi hao wabadilike na wawe tayari kuwapokea watumishi wenzao watakaowasili kwa awamu kuanzia mwezi huu.
Huduma za afya
Asubuhi akitembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa ameridhika na maelezo aliyopewa na kuwataka watumishi wanaohamia Dodoma walionesha hofu ya kupata huduma ya afya, kuondoa shaka hiyo.
“Watumishi wanaohamia Dodoma wafahamu kuwa hakuna shida ya matibabu ya huduma za afya hospitali zipo zina huduma nzuri,” alisema na kutaka pia kuimarishwa kwa zahanati na vituo vya afya.
Hata hivyo Mganga Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk James Charles akitoa taarifa yake kwa Waziri Mkuu alisema hospitali hiyo inafaa kupewa kipaumbele ili iweze kutoa huduma zake kutokana na kuhudumia watu milioni 2.3 kwa mwaka ambao wanatoka katika mikoa ya Dodoma, Singida, Iringa, Manyara na Tabora.
“Imekuwa kama hospitali ya rufaa kwani kuna huduma ya upasuaji wa mifupa na kuna madaktari bingwa wanaotoa huduma nzuri... tunaomba hospitali hii ipewe hadhi ya hospitali ya kanda maalumu kwani inahudumia wagonjwa wengi na kwa mwaka zaidi ya wagonjwa 6,000 hufanyiwa upasuaji,” alisema.
Dk Charles alisema ujio wa serikali Dodoma kama mkoa wamejiandaa kutoa huduma nzuri pia ikizingatiwa kuna hospitali kubwa tano ikiweno hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa, hospitali ya Dodoma Christian Medical Centre (DCMC), hospitali ya Mirembe na St Gema ambayo ni hospitali teule ya manispaa ya Dodoma.
Biashara ya masoko
Akizungumza katika soko kuu la majengo, Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara kujipanga kutokana na ujio wa serikali Dodoma ambapo watumishi 2,700 watahamia mkoani humo.
Alisema watumishi hao watahamia na familia zao na hivyo ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara kuboresha huduma zao na kuongeza kuwa uhamiaji huo utakuwa wa awamu sita. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, soko kuu linatakiwa kuwa na mipango ikiwemo sehemu maalumu ya kuegesha magari.
“Wageni mashuhuri watakuja Dodoma, mabalozi watajenga ofisi Dodoma, na mataifa ya nje yatakuja Dodoma,” alisema.
Aidha baada ya kusoma mabango ya malalamiko katika mazungumzo yake Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wa Soko la Majengo ambayo imepanda kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 150,000 kwa mwezi.
Ujenzi Dodoma
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali yote itakuwa Dodoma ifikapo Juni 2020 ambapo jumla ya watumishi 2,700 watakuwa tayari wamehamia Dodoma. Aliitaka pia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuondoa nyumba zilizojengwa kiholela katikati ya mji pamoja na zile zilizojengwa kwa udongo.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na watumishi wa serikali na taasisi mbalimbali za serikali mkoani hapa na kuwataka watumishi hao kuwa na imani na serikali yao.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema kundi la kwanza la mawaziri linatakiwa kuwa Dodoma mpaka ifikapo Februari 28, 2017 wakati kundi la pili lilitatakiwa kuwa limefika Machi hadi Agosti 2017 na kufuatiwa na makundi mengine kama ilivyopangwa.
“Kila katibu mkuu atakapofika awe ameandaa mkakati wa kuleta watumishi Dodoma. Ili wizara zitenge fedha kwenye bajeti ya kuleta watumishi na kuwalipa stahiki kabla ya kuhamia Dodoma na Juni 2020 Serikali yote itakuwa imehamia Dodoma,” alisema na kuongeza kuwa huduma zote za serikali hasa za waziri mkuu zitapatikana Dodoma.
Alisema Rais John Magufuli aliahidi serikali yote itahamia Dodoma mpaka ifikapo 2020 na sasa serikali iko Dodoma na kuitaka mamlaka ya ustawishaji makao makuu (CDA) kutoa viwanja kwa wahitaji ili wajenge nyumba.
“Kamilisheni waraka na mkamilishe mchakato na Benki ya TIB ili hadi ifikapo Novemba viwanja vipimwe na watu wapate viwanja. Kuna kazi ya kubadilisha mji ili uendane na makao makuu ya serikali, tumeunda timu ya watu 10 kufanya ‘master plan’ ya mji wa Dodoma na watatoa mapendekezo yao, tunataka tusirudie kupanga mji kama tulivyofanya Dar es salaam kuwe na barabara tatu zinaingia na tatu za kutoka,” alisema.
Alisema kama kuna eneo la kujenga ghorofa CDA waseme eneo lipi kwa ajili ya maghorofa ili watu wajenge na waseme njia ya malori ili yasiweze kupita katikati, vile vile kama kunahitajika kujenga Mall wasirudie kosa la Dar es Salaam.
Waziri Mkuu alisema serikali pamoja na kazi yote iliyonayo inahitaji watumishi waadilifu na kutaka watumishi wa Dodoma wawe tayari kuwapokea wenzao na kuwataka wabadilike.