WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kuwekeza mkoani Dodoma na serikali imejipanga kutoa ardhi na kupunguza urasimu katika utoaji wa leseni.
Pia alisema serikali inaunga mkono juhudi za wawekezaji katika sekta ya viwanda na kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa sambamba na kutekeleza azma yake ya kuendeleza viwanda nchini ili taifa liweze kupiga hatua na kufikia uchumi wa kati.

Waziri Mkuu, Majaliwa alisema hayo jana wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza magodoro cha Dodoma Asili cha mjini hapa na Kiwanda cha Premalt Limited.
Waziri Mkuu alisema serikali imefungua milango kwa wawekezaji wanaotaka kujenga viwanda, nyumba za kuishi, kukodisha kama ofisi masoko makubwa, maeneo ya bustani ya kupumzika na uwekezaji mwingine na serikali itawaunga mkono.
“Ni jukumu lenu Watanzania kuja kuwekeza Dodoma milango iko wazi. Serikali hii itawaunga mkono wawekezaji wote wanaotaka kuwekeza Dodoma, wale wanaofikiria serikali haina nia njema na wafanyabiashara wajue hatuhitaji kuweka siasa sana kwenye utendaji,” alisema Majaliwa.
Alisema serikali inawapenda sana wafanyabiashara imejipanga vizuri katika kutoa ardhi na kupunguza urasimu katika utoaji wa leseni.
“Hatutaki kuweka siasa sana kwenye utendaji, sehemu kubwa ya ahadi ya Rais John Mgufulini kuhakikisha wananchi wanapata tija ya kuhudumiwa na serikali yake tatizo kubwa siasa imewekwa mbele sana,” aliongeza.
Alisema Dodoma Asili ni kiwanda chenye kuzalisha magodoro yaliyo bora yenye heshima na kuwataka watumishi wanaohamia Dodoma wasihame na magodoro kwani Dodoma kuna kiwanda chenye ubora.
“Watumishi wanaokuja Dodoma hawana haja ya kuhama na magodoro,” alisema Majaliwa aliyehamia mjini hapa mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Haidary Gulamali alisema kati ya wafanyakazi 150 walioajiriwa kiwandani hapo, 147 ni Watanzania na watatu ni wataalamu ambao ni raia wa kigeni. Alisema magodoro ya kiwanda hicho yamekuwa na soko zuri kutokana na ubora wake.
Alisema pia anakusudia kuanzisha kiwanda kikubwa cha kukamua mafuta ya alizeti ambacho kitakuwa na uwezo wa kukamua tani 100 kwa siku, ambapo kwa mwezi zitakamuliwa tani 3,000. Alisema mradi huo mpya unatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni nne.
Katika kiwanda ya kuzalisha unga wa kutengenezea gypsum kinachomilikiwa na mwekezaji kutoka India, Arnod Chandra, Waziri Mkuu alisema serikali itaangalia jinsi ya kuweka kodi kwenye bidhaa hiyo inayoingia kutoka nje ya nchi ambayo haitozwi kodi.