Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania na Rais
wa Taasisi ya Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza Fernandez de la
Vega, akisalimiana na maofisa wa ulinzi na usalama mara baada ya kuwasili
katika bandari ya Nansio, Ukerewe hivi karibuni kuzindua mradi wa kilimo cha
viazi lishe unaofadhiliwa na taasisi yake ya inayoshughulikia maendeleo ya
Wanawake wa Afrika.

Mama Getrude Mongella (waliosimama katikati mwenye blauzi nyekundu) akifafanua jambo kwa Mkamu wa Rais mstaafu wa Hispania na Rais
wa Taasisi ya Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza Fernandez de la
Vega, wakati walipotembelea mradi wa kilimo cha viazi lishe wilayani Ukerewe. Kushoto kwa Mama Mongella ni Bi. Leocadia Vedastus, ambaye ni mshiriki kiongozi wa mradi huo.
Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania na Rais
wa Taasisi ya Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza Fernandez de la
Vega, akiangalia bidhaa zilizo mbele yake ambazo zinatokana na viazi lishe katika kuongeza mnyororo wa thamani. Hii ni wakati alipokwenda kuuzindua mradi huo wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza.

MRATIBU wa mradi wa akinamama wapambanao na mazingira wa Green
Voices, Alicia Cebada, amesema kwamba wamefarijika na mradi huo kwa kuwa
umeonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania.


Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yao ya kutembelea
miradi mitano kati ya 10 inayotekelezwa na wanawake wa Tanzania,hivi karibuni
mratibu huyo kutoka taasisi ya Women for Africa Foundation, alisema
hawakutegemea kama miradi waliyoianzisha akinamama hao ingeweza kufanikiwa
katika kipindi kifupi tangu kuwapatia mafunzo.
“Ni kipindi kifupi tangu wanawake hawa walipopatiwa mafunzo
nchini Hispania, lakini kwa hakika miradi waliyoibuni imeonyesha mafanikio, ni
endelevu, rafiki wa mazingira na italeta tija kwao na taifa kwa ujumla,”
alisema Alicia.
Aidha, alieleza kwamba, changamoto pekee ambayo ipo mbele yao
ni kuhakikisha miradi hiyo inasimama na kuwafundisha wanawake wengi kadiri
wawezavyo ili kuhakikisha wanajiletea maendeleo katika maeneo yao kiuchumi na
kijamii.
“Tumewaona wanawake wa Ukerewe wanavyolima viazi lishe na
kuongeza mnyororo wa thamani, tumewaona wanawake wa Kijiji cha Kitanga huko
Kisarawe wakiongozwa na ‘Malkia wa Muhogo’ Abia Magembe, tumewatembelea
akinamama wanaofuga nyuki kupambana na ukataji wa misitu huko Kisarawe, pia
tumewaona wanawake wa Morogoro namna wanavyokausha mboga na kuwa na uhakika wa
akiba ya chakula, na hapa (Bunju) tumeshuhudia jinsi kilimo cha uyoga kilivyo
na faida, ni miradi mizuri, endelevu na rafiki mkubwa wa mazingira,” alisema.


Alicia Cebada na Anna Salado wakiangalia
namna ya mifuko ya kupandikizwa uyoga inavyohifadhiwa kwenye mapipa wakati
walipotembelea kilimo cha uyoga Bunju hivi karibuni.


Picha ya pamoja na akinamama wafugaji nyuki
katika misitu ya Pugu na Kazimzumbwi wilayani Kisarawe.

Alicia alisema kwamba, taasisi yake inaangalia uwezekano wa
kuwaongezea nguvu akinamama wa Green Voices katika awamu ya pili ya mradi baada
ya kuridhishwa na mafanikio ya majaribio ili waweze kukabiliana na changamoto
walizonazo.
Hata hivyo, aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono
mradi huo na akasema hiyo inawapa nguvu hata wanawake wanaoshiriki na ni dalili
njema kwamba wengi wanaweza kujifunza na kuitekeleza miradi kama hiyo na kubuni
mingine yenye manufaa kwa jamii.
“Tumeona jinsi serikali ilivyo bega kwa bega na wanawake hawa
katika sehemu zote tulizotembelea, hii inaonyesha kwamba miradi waliyoibuni
siyo yao pekee bali ya jamii nzima na itawahamasisha wanawake wengi zaidi
kujifunza na kuitekeleza katika maeneo yao,” alisema.
Kauli ya Alicia imekuja muda mfupi baada ya rais wa mfuko huo,
Mama Maria Tereza Fernandez de la Vega kuzuru nchini kushiriki uzinduzi wa
mradi huo Julai 11, 2016 ambapo ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.
Mama Samia aliahidi wakati wa uzinduzi kwamba serikali yake
itahakikisha inakuwa bega kwa bega kusaidia miradi hiyo iwe endelevu ili kuunga
mkono juhudi za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi,
kuongeza uhakika wa chakula, kuwakwamua wananchi na umaskini pamoja na kuongeza
ajira, hasa kwa wanawake.
Kwa upande wake, Mama Maria Tereza, ambaye ni makamu wa rais
mstaafu wa Hispania, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za akinamama wa
Tanzania na kusema kwamba taasisi yake inaangalia namna ya kuwasaidia zaidi.
“Tumefarijika sana na jitihada hizi, tumesikia changamoto
zinazowakabili na tutaangalia namna gani ya kuwasaidia kuzikabili katika awamu
ya pili ya mradi huu wa Green Voices,” aliwaeleza akinamama wa Ukerewe mbele ya
wananchi waliokusanyika katika eneo la Shule ya Bukongo.
Mkurugenzi wa ubunifu wa taasisi hiyo, Noellia, aliwapongeza
wanawake wanaotekeleza miradi hiyo kupitia Green Voices na kuwataka waendelee
kushikamana ili kusonga mbele huku akiwapa moyo kwamba changamoto zilizopo
zinaweza kutatuliwa.
Noellia alisema kwamba, kuonekana kwa changamoto ni dalili
njema kwamba kumbe miradi hiyo inatekelezeka ikiwa changamoto hizo zitafanyiwa
kazi.
“Kama unabaini vikwazo basi ni dalili kwamba kumbe vikifanyiwa
kazi unaweza kusonga mbele, msikate tamaa,” alisema wakati alipozungumza na
wanawake wafuga nyuki wilayani Kisarawe.
Naye mkurugenzi wa mawasiliano wa taasisi hiyo, Ana Salado,
alipongeza namna vyombo vya habari vilivyojitahidi kuripoti mafanikio ya wanawake
hao na kusema kwamba hali hiyo imesaidia kuihamasisha jamii kushiriki kutokana
na ukweli kwamba miradi yote iliyobuniwa na akinamama hao ina tija kwa taifa
zima.
Jumla ya wanawake 15 wa Tanzania walipatiwa mafunzo ya wiki
mbili jijini Madrid, Hispania mapema mwaka huu ambapo 10 kati yao walikwenda
kuanzisha miradi mbalimbali wakati watano ni wanahabari ambao wamekuwa
wakiripoti maendeleo ya miradi hiyo.
Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amesema kwamba mradi huo unatekelezwa
katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro,
Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro.
Anawataja wanawake
walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa watokayo vikiwa kwenye mabano – kuwa
ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani – Majiko Banifu), Abiah Magembe (Kisarawe,
Pwani – Usindikaji wa Muhogo na Mtama), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es
Salaam – Kilimo cha Uyoga), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji wa
Nyuki), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji wa Mboga na Matunda).
Wengine ni Farida Makame
(Kilimanjaro – Majiko ya Umeme-Jua), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza –
Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji
wa Nyuki), Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga),
na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo cha Matunda).
Kupitia miradi hiyo, zaidi ya
wanawake 300 wamepatiwa mafunzo mbalimbali huku program nyingine za mafunzo kwa
vitendo zikiendelea katika makundi yao.


Anna Salado akifurahi pamoja na akinamama
wa Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe. Wanawake hao wanajihusisha na mradi wa
usindikaji wa muhogo na mtama.


Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro,
Milikieli Mansweat Mahiku, naye aliongozana na viongozi wa taasisi ya Mfuko wa
Wanawake Afrika, Anna Salado (kushoto) na Alicia Cebada (wa pili kulia) kukagua
kilimo cha mboga mboga katika Kata ya Mzinga kwenye manispaa hiyo. Wa tatu
kushoto ni Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Secelela Balisidya, na
aliyeinama ni mshiriki kiongozi wa mradi wa ukaushaji mboga na matunda wa
Mzinga, Esther Muffui.

Kuendelea kwa miradi hiyo
kumeonyesha dalili njema hasa baada ya serikali kuahidi kuiendeleza kwa
kushirikiana na wanawake hao, ikiwa ni pamoja na kuangalia fedha za maendeleo
kupitia mfuko wa wanawake na vijana katika kila halmashauri.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe,
Estomih Chang’a, alikwenda mbali zaidi baada ya kuwashauri wananchi wa wilaya
hiyo kujikita katika kilimo cha viazi lishe ili kuongeza akiba ya chakula na
kukabiliana na baa la njaa.
“Ninashauri wananchi wote wa
Ukerewe kulima viazi lishe kwa sababu mbali ya kuongeza akiba ya chakula,
lakini vinaongeza pato la familia na taifa hasa vikichakatwa ili kutoa bidhaa
mbalimbali,” alisema.
Naye mjumbe wa bodi ya
taasisi hiyo, Balozi Getrude Mongella, akizungumza katika uzinduzi huo kwenye
viwanja vya Shule ya Msingi Bukongo mjini Nansio, aliwaomba watendaji wa
serikali kusimamia kidete mradi huo ili kuondoa njaa katika visiwa vyote vya
wilaya ya Ukerewe.
Alisema kwamba, kuanzishwa
kwa mradi huo wilayani humo siyo tu kutawakwamua wanawake na wananchi wote,
lakini pia kunaifanya Ukerewe kuwa kiini cha usambazaji wa zao hilo katika
maeneo mengine ya Mkoa wa Mwanza.
“Ninawaomba watendaji wa
serikali ya wilaya hamasisheni zao hili lilimwe katika visiwa vyote na kama
ilivyokuwa zamani ambao mbegu zote za pamba zilitoka Ukerewe, basi tengenezeni
na zalisheni mbegu za kutosha msambaze katika wilaya nyingine za Mkoa wa
Mwanza.
“Naamini mkoa wote ukilima
zao hili njaa haitakuwepo na wanawake wanaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali
ambazo wakiziuza zitawakwamua kiuchumi,” alisema.
Naye Naibu Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mh. Selemani Jaffo, ambaye pia
ni Mbunge wa Kisarawe, amesema yuko tayari kushirikiana na wanawake wanaosindika
muhogo katika Kijiji cha Kitanga pamoja na wilaya nzima ya Kisarawe kuhakikisha
wanajikwamua kiuchumi kutokana na zao hilo.
Aidha, Naibu Meya
wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku, alisema atahakikisha
anasimamia kwa bidii ili teknolojia ya ukaushaji wa mboga na matunda isambae kwa
wanawake wote wa manispaa hiyo.
Aidha, aliahidi
kwamba, yeye na madiwani wenzake watahakikisha asilimia 10 ya fedha za
maendeleo katika halmashauri wanapatiwa wanawake na vijana wanaofanya miradi
endelevu yenye tija na inayolenga kutunza mazingira kama wanavyofanya wanawake
hao wa Mzinga.
“Sasa hivi bajeti
ya maendeleo ya halmashauri imeongezwa hadi asilimia 60, sasa kati ya fedha
hizo, asilimia 10 ni miradi ya wanawake na vijana, ambayo kama tutaisimamia
vyema na kuielekeza kwenye miradi endelevu kama hii italeta tija.
“Kama wahisani hawa
wamejitokeza na wamekuja kutoka Hispania, sisi kama serikali nasi tunapaswa
kuunga mkono jitihada hizi ambazo zina tija kubwa,” alisema Naibu Mstahiki
Meya.