MTOTO wa umri wa mwaka moja, Issa Simbeye aliyekuwa akiishi na wazazi wake katika kijiji cha Chombe wilayani Sumbawanga, amekufa, watoto wengine watatu wakiwemo ndugu zake wawili wako mahututi baada ya kula njegere pori.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema tukio hilo ni la Oktoba 8, mwaka huu, saa 12 jioni katika kijiji cha Chombe, kata ya Kaoze wilayani Sumbawanga ambapo watoto hao walienda porini kutafuta mboga kwa ajili ya chakula.

Aliwataja watoto wengine ambao wamelazwa katika Zahanati ya Chombe kwa matibabu kuwa ni Sara Simbeye (4) na Aderick Simbeye (6) ambao ni ndugu wa familia moja na marehemu.
Mtoto mwingine aliyelazwa ni Erick Tobiti (10) naye mkazi wa kijiji hicho. Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, wakizungumza kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini, kwa nyakati tofauti walisema kuwa watoto hao walikwenda porini kuchuma mboga pori za majani zinazofanana na njegere, ambapo walipika na kula kutokana na kushinda njaa kutwa nzima.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda Kyando alidai kuwa siku ya tukio watoto hao walienda porini, ambapo walichuma njegere pori kisha jioni wakapika na kula muda mfupi baadaye watoto hao walianza kutapika na kuishiwa nguvu ambapo mtoto Issa alipoteza maisha akipelekwa zahanati kwa matibabu.
Kamanda alisema uchunguzi wa awali, umebaini kuwa chanzo cha kifo cha mtoto huyo na wengine kudhurika ni kula njegere pori zinazosemekana ni sumu. Amewaasa wazazi kuwa makini katika malezi ya watoto wao kwa kuwapatia mahitaji yao ya msingi ikiwemo chakula.