Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akipanda mti jijini Dar es Salaam
WATANZANIA wametakiwa kupanda miti nchi nzima kwa lengo la kuondoa hewa ukaa ambayo imechangia mabadiliko ya tabia ya nchi.
Akizindua kampeni ya mti wangu jana Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema kuwa baada ya binadamu kuharibu mazingira kinachotokea ni adhabu.

“Ninukuu usemi wa Baba Mtakatifu Francis alipokuwa akizungumza katika mkutano wa pili wa lishe mwaka 2014, alisema kuwa binadamu anapofanya dhambi, anatubu na kusamehewa, lakini ukifanya makosa ya mazingira hayawezi kukusamehe,” alisema Mama Samia.
Alisema pia kuwa matokeo ya makosa ya kimazingira ni joto kali, mafuriko na kwamba kila Mtanzania anatakiwa kurekebisha makosa hayo ili mazingira yawe rafiki badala ya adui.
Samia alisema kama kupanga ni kuchagua, basi kila mtu anatakiwa kuenzi mazingira ili nayo yaweze kuwaenzi kwa kurudisha hali ya misitu na kufafanua kuwa mabadiliko ya tabia nchi husababishwa na kuharibiwa mazingira kwa shughuli za binadamu ikiwemo viwanda.
“Nikiwa mlezi wa mazingira ningependa kampeni hii iwe nchi nzima. Tumepanda miti 20,000 katika mkoa huu na kila mmoja anao wajibu wa kuutunza na ili kuleta mandhari nzuri kwa mkoa huu,” alisisitiza.