Samsung imetangaza kwamba haitaunda tena simu aina ya Galaxy Note 7 baada ya kutokea kwa ripoti kwamba simu ambazo kampuni hiyo iliamini ziko salama zinawaka moto.
Kampuni hiyo ya Korea Kusini ilikuwa tayari imepunguza uundaji wa simu hizo na mapema leo ikawataka waliokuwa na simu hizo kuzizima na kuacha kuzitumia huku uchunguzi ukiendelea.

"Samsung imeacha kabisa uundaji wa simu za Galaxy Note7," kampuni hiyo imeambia BBC.
Waliokuwa tayari wamenunua Galaxy Note 7 wanatarajiwa kuzirejesha kwa kampuni hiyo na kurejeshewa pesa zao au wapewe simu aina nyingine za Samsung.
Kampuni hiyo ilikuwa awali imetangaza kwamba ingesitisha uuzaji wa simu hizo.
"Majuzi, tulipunguza kiwango chetu cha uundaji wa simu hizi kuwezesha uchunguzi wa kina na uangalizi kwenye ubora wake, lakini kwa sababu tunatilia maanani sana usalama wa wateja, tumefikia uamuzi wa mwisho wa kusitisha uundaji wa Galaxy Note 7s," kampuni hiyo imesema.
Samsung iliwataka watu waliokuwa wamenunua jumla ya simu 2.5 milioni mwezi Septemba kuzirejesha madukani baada ya wateja wengi kulalamika kwamba betri za simu hizo zilikuwa zinalipuka.
Walipewa simu mpya ambazo zilidaiwa kuwa salama.
Lakini sasa taarifa zimetokea kwamba hata simu hizo zilizodaiwa kuwa salama zinashika moto.
Hisa za kampuni hiyo leo zimeshuka asilimia 8 katika soko la hisa la Seoul.
Mwanamume mmoja jimbo la Kentucky, Marekani anasema aliamka na kupata chumba chake cha kulala kimejaa moshi uliotokana na simu mpya ya Note 7 aliyokuwa ameipata baada ya kurejesha ya awali.
Siku chache awali, abiria kwenye ndege moja Marekani walitakiwa kuondoka kwa dharura ndegeni baada ya simu ya Note 7 kuanza kutoa moshi.