Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Oct 13, 2016

Shehena ya mafuta ya kula yanaswa Tabata

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamekamata shehena ya mafuta ya kula ambayo hayajalipiwa kodi wala kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutumika kwa walaji.
Kamanda wa Polisi Kanda hiyo Maalumu, Simon Sirro, amewaeleza waandishi wa habari leo kuwa, shehena hiyo ilikamatwa baada ya kufanyika kwa operesheni ya kuwasaka wakwepa kodi wanaoingiza bidhaa nchini kwa magendo kinyume cha sheria za nchi.

Amesema Oktoba 10 huko maeneo ya Tabata Ubaya Ubaya, karibu na Chuo cha St Mary’s, askari walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Proches Shayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna mafuta ya magendo yamepitishwa kupitia ufukwe wa Bahari ya Hindi, Mikocheni maeneo ya Mlalakua.
Ameongeza kuwa askari wakishirikiana na maofisa wa TRA walifanya ufuatiliaji mzigo ulipopelekwa ndipo wakagundua mafuta yamepelekwa maeneo ya Tabata na walipofika nyumbani kwa Shayo, walifanya upekuzi na kufanikiwa kukamata mafuta ya kula yenye lebo ya Safi na Oki, madumu 453 ya lita 20 ya thamani ya Sh 14,296,680.
Amesema katika mahojiano, mtuhumiwa alishindwa kuthibitisha uhalali wa umiliki wa mafuta hayo na kushindwa kutoa nyaraka muhimu. Upelelezi unaendelea na utakapokamilika, mtuhumiwa atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutaifishwa bidhaa husika.
Katika tukio lingine, Polisi Kanda maalumu, Oktoba 12, mwaka huu maeneo ya Kimara Temboni, wamekamata vifaa bandia vya kutengeneza pombe aina ya Konyagi.
Amesema hatua hiyo ya kukamata vifaa hivyo, polisi walipata taarifa kwa msiri kuwa kuna watu wana vifaa bandia vya kutengenezea pombe bandia aina ya Konyagi na baada ya kufuatilia walikuta vifaa hivyo vikiwa vimetelekezwa.
Vifaa hivyo ni mashine moja ya kujaza na kufunga pombe ya viroba aina ya Konyagi, rola 57 za viroba, ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya kujaza pombe, madumu sita ya ujazo wa lita tano, kati ya hayo mawili yakiwa na dawa ya kutengenezea ladha ya kinywaji hicho na matatu yakiwa bila alama yoyote, na tepu ya kufungia maboksi.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP