Abiria wakigombea kuingia kwenye basi la mwendokasi eneo la Manzese, Dar es Salaam hivi karibuni. (Picha ya Maktaba).
LICHA ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika utoaji huduma wa magari yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (DART), Kampuni inayoendesha mradi huo, UDART imepiga marufuku usafiri wa bure kwa makundi mbalimbali wakiwemo askari polisi, walemavu, viongozi wa dini na hata walimu.

Imesema mageti yaliyokuwa wakiyatumia yafungwe na kila mmoja alipe. Udart imetoa taarifa hiyo katika waraka uliobandikwa katika kila kituo mwishoni mwa wiki na kufafanua kuwa kumekuwepo na ongezeko la makundi hayo, wakipita katika mageti hayo bila kulipa na pia kupokea simu kutoka katika makundi mbalimbali, yakiomba kupatiwa huduma hiyo.
Hilo limo katika waraka uliosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UDART, David Mgwassa na nakala kwenda kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Msajili wa Hazina na kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).
Katika taarifa hiyo, Mgassa alitaka waraka huo ufike kwa watumishi wote wa usafiri huo na hatua zichukuliwe haraka. Alisema watumishi waliopo katika vituo wanapaswa kuhakikisha mageti yanakuwa yamefungwa kwa ufunguo na hakuna anayeruhusiwa kupita bila kulipa.
Makundi hayo yalikuwa yakisafiri bila kulipa nauli katika mradi huo unaofanya kazi katika Barabara ya Morogoro na ile ya Morocco jijini Dar es Salaam.
Changamoto nyingine
Aidha, kumekuwapo na changamoto kadhaa ambazo zimeonekana kuwa sugu kwa sasa katika mradi huo ulioanza mapema mwaka huu; ambazo ni magari kuchelewa kufika vituoni kwa zaidi ya nusu saa, jambo linalosababisha abiria kupoteza muda mwingi na mengine yafikapo kutosimama vituoni.
Changamoto nyingine ni ya abiria ambao wanatumia kadi wanapoweka fedha, hutumika kwa safari chache, ikilinganisha na kiasi cha fedha kilichowekwa.
Kutokana na hali hiyo, watumiaji wake wamekuwa wakilalamikia mradi huo siku hadi siku kwamba tangu ulipoanza umekuwa tofauti na matarajio ya abiria kwa kadri siku zinavyokwenda, kwani umekuwa ni wa kupotezea abiria muda badala ya kuuokoa.
Mbali na hilo, mashine za kukagua tiketi na kadi zinazotumika katika usafiri huo, nazo zimekuwa na kero mbalimbali, nyingine zikichelewesha na nyingine zikigoma, jambo linalosababisha kuwepo kwa msururu wakati wa kuingia kwa abiria na kutoka.
Mtendaji Mkuu wa Mradi huo, Ronald Lwakatare alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa wanapopata malalamiko huyatafutia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Lwakatare alisema kuchelewa kwa magari vituoni hilo ni kosa na kwamba madereva wanapoulizwa wanasema kuwa tatizo ni uwepo wa askari wa usalama barabarani wanaoongoza magari, jambo ambalo huchelewesha kuyaruhusu magari hayo, jambo ambalo hubadili mfumo mzima wa usafiri huo.
“Ni kweli kwamba mradi huu umeanza mapema mwaka huu, lakini mpaka sasa haujatengemaa. Magari yanatakiwa kufika kituoni kila baada ya dakika tano zaidi ya hapo hilo ni tatizo,” alisema Lwakatare na kuongeza kuwa mfumo wa barabara pia huchangia mabasi kuchelewa kufika kituoni.
Alifafanua kuwa magari hayatakiwi kufika kituoni zaidi ya matano kwa wakati mmoja na hali hiyo husababishwa na askari ambao wanaongoza magari ama kuwepo kwa msafara wa aina yoyote ile. Alisema wamekuwa wakishirikiana na askari kuhakikisha magari hayo, yanapewa kipaumbele ili yawe na maana kwa watumiaji kama yanavyoitwa.
Lwakatare alisisitiza magari yaliyopo ni 120 na kwamba sio magari yote hayo yanafanya safari kwa siku moja, kwa kile alichoeleza kuwa yanapishana kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo kwa kadri yanavyoharibika.
Vilevile aliongeza kuwa kuna wakati magari yanakuwa yamesimama vituoni, bila ya kwenda mahali kwa kuwa madereva wake wanakwenda msalani au kula.
“Lengo la kufanya magari hayo yawe yanafika kituoni kila baada ya dakika tano ni kurahisisha usafiri, lakini abiria wanaposubiri magari zaidi ya nusu saa bila kupata huduma hilo ni kosa, tutalifanyia kazi,” alieleza Lwakatare, na kufafanua kuwa magari hayo huanza kazi saa 12 asubuhi.
Alieleza kuwa baadhi ya njia ikiwemo Kivukoni na Gerezani Kariakoo, zimepewa kipaumbele kwa kuwa na magari mengi kuliko njia ya Morocco.
Alisisitiza kuwa safari za asubuhi na jioni ni tofauti na ya mchana kwamba wanatoa magari mengi kuwapeleka watu kazini na kwa mchana hupunguza magari kutegemeana na siku kwani hutofautiana siku hadi siku.
Akizungumzia magari yanayoanzia Mbezi, Lwakatare alisema yapo magari 26 kwa ajili ya kuwatoa abiria walio nje ya Dar es Salaam kwenda Kimara ambapo ndio kituo kikuu na utaratibu wanaoutumia wa kupanga foleni ndipo abiria waingie kwenye gari, ndio utaratibu mzuri unaofundisha ustaarabu badala ya kugombania magari hayo.
Aidha, alisema wanategemewa na watumiaji wa usafiri kwa kuwa asilimia kubwa ya daladala zilizokuwa zinaenda Kariakoo na Posta kupitia Barabara ya Morogoro zimepungua. “Tutazifanyia kazi changamoto zote zinazojitokeza kwa lengo la kuboresha usafiri huu. Tunawaomba abiria wavumilie tunapozifanyia kazi changamoto hizi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, msemaji wa UDART, Deus Bugaywa alisema takriban asilimia 30 ya mabasi hayo hupunguzwa katika kutoa huduma hususani nyakati za mchana kutokana na muda huo kuonekana kutokuwa na abiria walio wengi ikilinganishwa na asubuhi ama jioni wakati wengi wakielekea majumbani.
Bugaywa alisema magari hayo yamegawanywa katika hatua mbalimbali wakati wa kutoa huduma ambao huanza kutoa huduma kuanzia alfajiri saa 11 hadi saa nne ikiwa ni muda ambao abiria ni wengi vituoni na saa nane mchana hadi saa tatu usiku.
“Hata hivyo, muda mwingine magari hayo huendelea kutoa huduma hadi saa sita usiku na mpishano wa basi kwa basi ni dakika tano, na katika siku za Jumamosi na Jumapili magari hupunguzwa ili kutoa muda wa matengenezo,” alisema na kuongeza kuwa matengenezo mengine makubwa hufanyika kuanzia saa tano usiku hadi asubuhi.
Alikiri ni kweli kuwa changamoto katika huduma hiyo zipo zikitofautiana, lakini zikiendelea kufanyiwa kazi siku hadi siku, lengo likiwa ni kuifanya huduma hiyo kuwa bora yenye kufanikisha kiu ya watumiaji.