Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
SERIKALI imesema kwamba dawa muhimu za binadamu zinapatikana kwa wingi katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa saa 24 zikiwemo dawa za kutibu malaria, kifua kikuu, ukoma, kufubaza makali ya Ukimwi, dawa za kutuliza maumivu pamoja na anti-biotic ili kutimiza na kutekeleza Sera ya Mpango wa Afya wa Awamu ya Tano.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam jana ili kuzungumzia hali ya upatikanaji wa dawa na chanjo nchini.
“Dawa zote muhimu kwa binadamu zinapatikana kwenye Bohari Kuu ya Dawa kwa saa 24 kinyume cha watu na taasisi zisizo za kiserikali kusambaza maneno kuwa MSD imeishiwa dawa, kitendo ambacho sio cha kweli dawa zipo na zinasambazwa kwenye vituo vyote vya afya,” alisema Ummy.
Aidha, Ummy alisema ili kutekeleza Mpango wa Sera ya Afya wa Serikali ya Tano jumla ya Sh bilioni 251 zimetengwa ili kuhakikisha dawa za binadamu zinapatikana kila wakati pindi zinapohitajika kutoka MSD ili kutoa huduma bora kwa Watanzania.
Aliongeza kuwa serikali imetenga Sh bilioni 85 kwa ajili ya kulipa deni linalodaiwa na MSD ili kuhakikisha bohari hiyo, inajiendesha vizuri na kutokuwa dawa pindi zinapohitajika katika vituo vya afya na kutoa huduma za matibabu kwa muda muafaka kwa Watanzania.
Mbali na hayo, waziri huyo alisema tatizo la chanjo kwa sasa limepata ufumbuzi, kwani imenunua na kupokea chanjo za watoto za kifua kikuu dozi milioni mbili, chanjo za pepopunda dozi milioni 1.2 na chanjo za polio ambazo ni dozi milioni 2 ili kuimarisha hali ya matibabu nchini.
“Tulikuwa na tatizo la chanjo kama wiki nne zilizopita, lakini tumejitahidi na tumeweza kuleta chanjo zote muhimu pamoja na kuagiza chanjo za surua ambazo zinatarajiwa kuwasili hivi karibuni ili kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wingi nchini,” alieleza na kuongeza kuwa wanahitaji kununua na kufanya uzalishaji wa dawa katika viwanda vya ndani ili kuchangia uchumi wa viwanda vya ndani ili tufikie uchumi wa kati.
Aidha, aliwataka wakurugenzi wa vituo vya afya pamoja na waratibu wa afya wa wilaya, kuagiza dawa MSD mapema bila ya kusubiri ziishe kwenye vituo vyao ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.