Wabunge nchini Burundi wamepiga kura kujitoa katika mahakama ya kimataifa ya jinai ICC, na kushinikiza uamuzi wa baraza la mawaziri wiki iliopita wa kukatiza ushirikiano na mahakama hiyo iliopo The Hague-Uholanzi.

Kura hiyo inajiri miezi sita baada ya mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda kusema atachunguza ghasia nchini Burundi.
Ghasia za kisiasa zilianza April 2015 baada ya rais Pierre Nkurunzinza kuanza azma yake ya kuhudumu kwa muhula wa tatu.
Tangu hapo zaidi ya watu 400 wameuawa katika ghasi hizo na zaidi ya watu 200,000 wameyakimbia makaazi yao.