Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa muda wa miezi miwili kwa wafanyabiashara wanaotumia majina ya biashara pasipo kusajiliwa, wafanye hivyo haraka.
Baada ya muda huo kupita, patakuwa na msako nchi nzima ili kuwabaini wale wote wanaotumia majina ya biashara pasipo kusajili na kuwafikisha katika vyombo vya sheria au kuwatoza faini.

Akizungumza na waandishi wa jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi alisema katika kazi hiyo ya kutoa elimu na kurasimisha majina ya biashara na kampuni inayoendelea katika mikoa mbalimbali, imebainika kuwa wafanyabiashara wengi wanatumia majina ya biashara pasipo kuyasajili.
“Sheria ya Majina ya Biashara inamtaka mfanyabiashara kusajili jina la biashara yake ndani ya siku 28 toka aanze kulitumia,” alisema Kanyusi na kuongezea kuwa kinyume cha hapo atakuwa amevunja sheria ya majina ya biashara.
Alisema sasa usajili wa majina ya biashara umerahisishwa, kwani unafanywa kwa njia ya mtandao kwa kutembelea tovuti ya wakala huo ambayo ni www.brela.go.tz ili kupata maelezo yote ya namna ya kusajili jina la biashara.
Aliwataka wafanyabiashara wasiishie kusajili tu jina la biashara, bali pia waende katika Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa ajili ya kupata Namba ya Mlipa Kodi (TIN), pia waendelee katika halmashauri zao kupata leseni ya biashara.
“Kwa kurasimisha biashara serikali itapata mapato kwani wigo wa walipa kodi utaongezeka na pia itakuwa faida kwa wafanyabiashara katika kujengewa mazingira bora ya kufanya biashara,” alisisitiza Kanyusi.
Alisema Brela imejipanga kuzunguka mikoa yote nchini ili kutoa elimu juu ya urasimishaji wa majina ya biashara na kampuni kwani imeonekana wananchi hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa urasimishaji.
Hadi sasa Brela imefanya ziara katika mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Simiyu na wiki hii watakuwa mkoani Shinyanga kwa wiki moja katika kuhamasisha wafanyabiashara kurasimisha biashara zao.
Alisisitiza kuwa ni lazima kuhakikisha kuwa biashara zinarasimishwa ili serikali iwatambue walipa kodi wake ambao watachangia Pato la Taifa na kuiwezesha Tanzania kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.