WATAFITI wawili na dereva mmoja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian (SARI) jijini Arusha wameuawa na kisha miili yao kuchomwa moto katika kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino katika mkoa wa Dodoma wakati wakifanya utafiti wa udongo, baada ya kuhisiwa kuwa ni wanyonya damu.

Waliouawa wametajwa kuwa ni Nicas Magazine aliyekuwa dereva wa gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin lenye namba za usajili STJ 9570 mali ya Selian pamoja na watafiti wawili ambao ni Teddy Lumanga na Jaffari Mafuru.
Polisi mkoani Dodoma inawashikilia wanakijiji 30 wa kijiji cha Iringa Mvumi kuhusu mauaji hayo, huku Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana akitoa amri ya kuwasimamisha kazi Ofisa Utumishi wa Wilaya hiyo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.
Mauaji hayo yalitokea juzi katika kijiji cha Iringa Mvumi, tarafa ya Makang’wa wilayani Chamwino baada ya watu hao waliokuwamo katika gari hilo kuvamiwa na wanakijiji wa Iringa Mvumi na kuwakatakata kwa mapanga pamoja na silaha za jadi kisha kuwachoma moto hadi kufa. Inadaiwa chanzo cha tukio hilo ni Cecilia Chimanga (34) kupiga yowe kijijini kuwafahamisha kwamba ameona watu anaohisi ni wanyonya damu (mumiani).
Baada ya taarifa hizo kufika kijijini ndipo Mchungaji wa madhehebu ya Kanisa la Christian Family, Patrick Mgonela (46) alikitangazia kijiji kupitia kipaza sauti cha kanisani kuwa wamevamiwa na wanyonya damu ndipo wanakijiji wakaenda kuchoma gari, kuwaua na kuwachoma moto.
Baada ya tukio hilo, msako ulifanyika kwa kujumuisha askari wa kawaida na makachero na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na maofisa wengine wa Polisi. Akizungumza na gazeti hili jana Kaimu Ofisa Tarafa ya Makang’wa, George Mzuri alisema watafiti hao pamoja na dereva walifika kijijini hapo kufanya shughuli zao, lakini hata hivyo hawakupitia ofisini.
“Tunasikia walifika kijijini kwa ajili ya shughuli zao, lakini hawakutoa taarifa kwenye Serikali ya Kijiji wakawa wanatafuta njia ya kutokea wakafika mahali wakakuta akinamama wanaopika chumvi kwa njia ya asili,” alidai Mzuri.
Alisema waliamua kumwita mmoja wa wanawake hao ili wamuulize njia, lakini mama yule alikuwa akiogopa kwa kudhani kuwa walikuwa ni wanyonya damu.
“Mara yule mama akaanza kupiga kelele, karibu na hapo walipokuwa kuna kanisa ambalo likatumika kutangaza watu waelekee mbugani kuna wanyonya damu,” alisema na baada ya wananchi hao kufika eneo la tukio walianza kuwashambulia watu hao na kisha kuwaua na kuwachoma moto.
Alisema juhudi za kuwaokoa watu hao zilishindikana kutokana na wingi wa watu. Akizungumza katika eneo la tukio, Rugimbana alisema wote waliohusika na mauaji hayo watachukuliwa hatua za kisheria, wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema mpaka sasa watu 30 wanashikiliwa na Polisi wakiwemo wanaume 21 na wanawake tisa.
Jijini Arusha, Mratibu wa Utafiti wa Kituo cha Selian, Charles Lyamchai alisema, “ni huzuni kwetu sisi wafanyakazi wa Kituo cha Utafiti cha Selian Arusha mara baada ya kusikia vifo vya wafanyakazi wenzetu waliochomwa moto jana (juzi) wakiwa wanaendelea kufanya utafiti wa udongo huko mkoani Dodoma.
“Ukweli taarifa hizi zimetuumiza sana kwani wenzetu walikuwa wakifanya utafiti kwenye vijiji mbalimbali ili kujua aina za udongo unaofaa kwa ajili ya kilimo.”
Kwa mujibu wa Lyamchai, taarifa hizo zimewashtua wafanyakazi wa kituo hicho kwani wenzao walikuwa kazini wakitekeleza majukumu yao ya kazi.
Alisema wiki mbili zilizopita wenzao walikuwa wakiendelea na kazi ya kukusanya sampuli za udongo kwenye maeneo mbalimbali, lakini walipofika kijiji hicho cha Iringa Mvumi wakiendelea na shughuli, ghafla walitokea watu wasiojulikana na kuanza kupiga mayowe kisha kuanza kuchoma moto gari la serikali pamoja na watumishi hao watatu.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Nicas Magazine ambaye alikuwa ni dereva wa gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin yenye namba za usajili STJ 9570 mali ya Selian, pamoja na watafiti wawili ambao ni Teddy Lumanga pamoja na Jaffari Mafuru.
“Tumeumia na tukio hili, lakini ndio hivyo yameshatokea na baadhi ya wenzetu wameshaondoka kwenda mkoani Dodoma ili kujua tunaanzia wapi na kupanga taratibu za maziko, lakini tumeshtushwa na tukio hili kwa kweli tumeumia sana,” alisema mratibu huyo wa Utafiti wa Selian.
Aliongeza kuwa kazi wanazofanya watafiti ni ngumu sasa hawajui kabla ya kukutwa na mauti hayo wenzao walikumbana na nini. Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Veronica Mheta, Arusha