Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Zanzibar, Mussa Aboud Jumbe
IDARA ya Maendeleo ya Uvuvi imetoa muda wa wiki kwa kamati za uvuvi za shehia kuimarisha mazingira ya usafi katika masoko yanayotumika kwa ajili ya kutoa huduma za kunadi samaki.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Mussa Aboud Jumbe alisema hayo wakati alipozungumza na viongozi wa kamati za shehia za uvuvi za Mkoa wa Kaskazini, ambazo zimebainika kwamba mazingira ya masoko yao yapo katika hali mbaya.

Jumbe alisema haikubaliki kuona mazingira ya masoko hayo yapo katika hali mbaya wakati biashara ya kunadi samaki ikifanyika na kuingiza fedha nyingi.
“Nazipa muda wa wiki moja kamati za shehia za uvuvi kuhakikisha zinaimarisha mazingira ya usafi wa masoko au vyenginevyo nitayafunga na kuacha kufanya biashara hiyo,” alisema Jumbe na kuyataja masoko ambayo yapo katika hali mbaya ni Matemwe, Kiwengwa pamoja na Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Baadhi ya wenyeviti wa kamati za uvuvi walidai kwamba wanahitaji fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya kutengeneza masoko hayo kutoka serikalini.
Mjumbe wa Kamati ya Uvuvi wa Kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mati Wadi alisema baadhi ya wavuvi wamelikimbia soko la kijiji hicho na kuuza samaki wao mjini kwa ajili ya kupata bei nzuri.
“Tunaiomba Idara ya Uvuvi kuweka sheria ambazo zitawafanya wavuvi wa kijiji hiki kuuza samaki wao nyumbani ili kusaidia kupata mapato ya kuendesha pamoja na michango mbalimbali ya kijijini hapo,” alieleza Wadi.
Baadhi ya wajumbe walitoa masikitiko yao na kutaka baadhi ya aina ya uvuvi kuruhusiwa kutumika ikiwemo bunduki ili kuzamia baharini na kutafuta mazao ya baharini.
“Baadhi ya wavuvi wanataka aina ya uvuvi kuruhusiwa kwa mfano uvuvi wa kutumia bunduki na kuzamia baharini kutafuta na kuvuna mazao ya baharini,” alisema Issa Iddi.