WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametangaza takwimu mpya za matumizi ya umeme na kueleza kuwa watu idadi ya Watanzania wanaotumia umeme imeongezeka hadi kufikia asilimia 67.5.
Kiwango hicho kimebainishwa katika utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Utafiti huo umefanywa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara kuanzia Oktoba hadi Novemba mwaka jana. Lengo la utafiti huo ilikuwa ni kuangalia hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme na idadi ya watu wanaotumia nishati hiyo.
Idadi hiyo imeongezeka maradufu. Kwa mujibu wa NBS, mwaka 2007 idadi ya watu waliokuwa wanatumia umeme hadi mwaka huo ilikuwa asilimia 10 ya Watanzania.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa asilimia 49.5 ya watumiaji wa umeme wako vijijini. Kiwango hicho cha wananchi wanaotumia umeme vijijini kimeongezeka kutoka asilimia mbili ya mwaka 2007.
Mwishoni mwa mwaka jana, NBS ilitangaza kuwa lengo la kufanya utafiti huo ni kukusanya takwimu rasmi zinazohusu hali ya upatikanaji wa nishati umeme katika ngazi ya jumuiya na kaya ili kujua matumizi ya umeme na nishati pamoja na faida zake kwa maendeleo.
Sanjari na ukusunyaji wa takwimu hizo, Dk Kwesibago alisema utafiti huo utahusisha ukusanyaji wa takwimu za kidemografia na za kiuchumi za wanakaya zikijumuisha umri, jinsia, hali za ndoa, elimu, shughuli za kiuchumi, matumizi ya muda pamoja na ushiriki wa jinsia katika shughuli za kiuchumi na kijamii.