Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Fredrick Sumaye
MWENYEKITI wa Kanda ya Pwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fredrick Sumaye amesema uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano umechukua hatua mbalimbali za kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali hususani katika Jiji la Dar es Salaam.

Aidha, Sumaye ambaye alishika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, amesema jitihada hizo zinatokana na jiji hilo kuwa na idadi kubwa ya viongozi wa upinzani akidai kuwa wametoa msukumo katika nyanja mbalimbali.
Sumaye alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia uchaguzi uliofanywa na chama hicho na yeye kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda hiyo, Makamu Mwenyekiti wa kanda hiyo akiwa ni Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea na Mweka Hazina akiwa Ruth Mollel ambaye pia ni mbunge wa chama hicho kupitia Viti Maalumu.
Kanda ya Kaskazini inaundwa na mikoa ya kichama ya Pwani, Ilala, Kinondoni na Temeke.
“Kwa Dar es Salaam, serikali imechukua hatua nyingi za kuleta maendeleo, mafanikio hayo yamefikia hapo kutokana na kuwepo kwa viongozi wengi ambao ni wapinzani,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa mafanikio hayo ni sifa kwa wapinzani.
Alisema popote penye viongozi wengi wa upinzani maendeleo yanakuwepo kwa wingi, na akiwaagiza wabunge, mameya, madiwani pamoja na wenyeviti wa mitaa ambao miradi mbalimbali imetekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano wawaelimishe wananchi namna ya kuwa karibu na miradi hiyo.
Sumaye alisema baada ya kanda hiyo kupata viongozi masuala ambayo watayafanyia kazi ni pamoja na kusimamia maslahi ya wananchi ili waweze kupata maendeleo, heshima utu utawale na kuangalia ukuaji wa demokrasia.
Alisema kazi ya vyama vya upinzani ni kuiambia serikali iliyoko madarakani ni kitu gani kinachotakiwa na ambacho wangekihitaji kiweze kufanyiwa kazi.