Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud
JUMLA ya watu 315 wakiwemo wafanyabiashara wamebainika kujishughulisha na mtandao wa dawa za kulevya huku 60 wakishikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud alisema hayo wakati akizungumza na Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Ofisi za viongozi wakuu wa Serikali ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Omar Seif Abeid.

Mahmoud alisema mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya ni kubwa na yenye mtandao mkubwa ambapo juhudi zinahitajika kuangamiza mtandao huo.
Alisema watu 19 tayari wamefunguliwa mashtaka katika mahakama za Unguja wakati polisi ikifanya uchunguzi zaidi dhidi ya watu 60 ambao wanadaiwa kujishughulisha na biashara hiyo.
Mahmoud aliieleza Kamati ya Baraza la Wawakilishi la viongozi wakuu wa Serikali kwamba ushirikiano mkubwa unahitajika katika kufaulu vita dhidi ya dawa ya kulevya ambapo vyombo vya ulinzi ikiwemo Polisi vinatakiwa kushirikishwa kikamilifu.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Ofisi za viongozi wakuu wa Serikali, Omar Seif Abeid alimpongeza mkuu wa mkoa kwa juhudi zake ambazo zimefanikiwa kuvunja mtandao wa dawa za kulevya na genge lake.
Alisema kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, tayari limepitisha azimio la kupambana na dawa za kulevya baada ya kuwasilishwa kwa hoja binafsi mbele ya Baraza.
Baadhi ya maeneo ambayo awali yalikuwa maarufu kwa biashara ya dawa hizo haramu ni Kundemba, Mji Mkongwe wa Zanzibar ikiwemo Malindi na Jangombe ambapo sasa magenge ya dawa za kulevya yameondoka.