Mwanasiasa mkongwe nchini, Chrisant Mzindakaya akizungumza na waandishi wa habari katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dar es Salaam. (Picha na Anna Nkinda, JKCI).
MWANASIASA mkongwe na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chrisant Mzindakaya amesema anashukuru Mungu afya yake inazidi kuimarika na kwamba taarifa zinazosambaa kwamba amekufa zipuuzwe.
Aidha, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha huduma katika hospitali mbalimbali nchini jambo ambalo linasaidia watu wengi kutibiwa nchini bila kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Mzindakaya alilazimika kuzungumza na vyombo vya habari baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana na juzi zikidai kuwa amekufa ambapo ametafsiri uvumi huo kuwa pengine watu wanamuombea maisha marefu.
Akiwa amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), waziri huyo wa zamani nchini aliwaambia waandishi wa habari kuwa amesikitishwa na taarifa hizo mbaya dhidi yake.
Alisema mtu ambaye anataka kutoa habari, ziwe na ukweli na kwamba hana haja ya kumshitaki mtu aliyesambaza habari hizo kwenye vyombo vya sheria zaidi ya kumshitaki kwa Mungu.
Aliwaasa Watanzania kuacha tabia ya kuropoka na kusambaza uongo wakidai ni uhuru wa habari.